2013-03-18 08:02:12

Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha moyo wa sala, tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma!


Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anabainisha kwamba, Kwaresima ni kipindi kinachotoa fursa kwa waamini kujikita zaidi katika maisha ya sala, kama njia ya kuzungumza na Mungu kutoka katika undani wa maisha yao. RealAudioMP3

Ni kipindi cha baraka kinachomwezesha mwamini kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza hija ya maisha mapya na kutembea katika mwanga wa Kristo mfufuka. Ni changamoto ya kumwongokea Mungu kwa kumwinulia akili na mioyo yao!

Katika mahojiano na Radio Vatican, Askofu Msaidizi Nzigilwa anakazia umuhimu wa kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha, kama njia ya kulitolea ushuhuda yakinifu. Tafakari ya Neno la Mungu ni sala endelevu katika maisha ya mwamini, inayopania pamoja na mambo mengine kumwezesha mwamini kupata ujumbe wa Neno la Mungu, ili uweze kumwongoza katika mapito yake ya kila siku.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa anasema Askofu Msaidizi Nzigilwa kujikita katika ushuhuda wa imani yao kwa njia ya matendo ya huruma yanayoonesha kwa namna ya pekee mshikamano wa Familia ya Mungu inayowajibika.

Si haba kwamba, Kwaresima waamini kwa namna ya pekee wanahamasishwa kupeleka huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili wao pia waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ikumbukwe kwamba, maskini na wahitaji wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ni wajibu na jukumu la Familia ya Mungu kuwaonjesha wahitaji upendo na huruma inayobubujika kutoka katika undani wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Matendo ya huruma yawasaidie waamini kushuhudia imani yao katika matendo, ili hatimaye, siku moja, waweze kufurahia maisha ya uzima wa milele.







All the contents on this site are copyrighted ©.