2013-03-18 12:13:56

Harambee kuchangia ukarabati wa Parokia ya Magomeni, Jimbo kuu la Dar es Salaam


Waziri mkuu Mizengo Pinda wa Tanzania, ameongoza harambee ya papo kwa papo na kufanikiwa kukusanya sh. milioni 31.5 zikiwa ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa la Parokia ya Mashahidi wa Uganda, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Akizungumza na waamini wa Parokia ya Magomeni, Jumapili, Machi 17, 2013, kabla ya kuendesha harambee hiyo, Waziri Mkuu aliusifu uongozi wa Parokia ya Magomeni kwa kuamua kufanya upanuzi wa Kanisa hilo ili liweze kuhudumia waamini wengi zaidi.

“Nia yao ni nzuri sana na wameona mbali mapema. Magomeni hii ya leo si ya wakati ule, na wala haitakuwa hivi katika miaka mingine 50 ijayo. Zamani usingeweza kuona hata ghorofa moja hapa Magomeni lakini sasa hivi maghorofa hayahesabiki,” alisema.

Aliwasisitiza waamini hao kujitoa kwa ajili ya kazi ya Kristo kwa sababu hakuna sadaka ambayo ni ndogo. “Hakuna sadaka iliyo ndogo mbele ya Mungu, kikubwa ni dhamira tu. Kanisa ni letu na litajengwa na sisi waamini ili mradi kila mmoja wetu aseme Kanisa hili nitalijenga,” alisisitiza.

Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waamini hao, Baba Paroko wa Kanisa hilo, Padri Sixfrious Rwechungura alisema wameanza kazi ya ukarabati tangu Agosti 15, 2011 na kwamba hadi sasa wamekwishakusanya sh. milioni 350 iliyotokana na nguvu za waamini wenyewe bila msaada wa kutoka nje.

Alisema wanahitaji kiasi cha sh. milioni 300 ili kukamilisha kazi hiyo ambayo inapaswa kukamilika katika miaka miwili ijayo ili iendane na maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Parokia ya Magomeni.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mkewe Mama Tunu Pinda waliahidi kuchangia sh. Milioni 10 na kutoa sh. Milioni mbili za kianzio. Pia aliendesha mnada wa mbuzi aliyenunuliwa kwa sh. 600,000/- na mkoba ulionunuliwa kwa sh. 150,000/-.









All the contents on this site are copyrighted ©.