Shutuma dhidi ya Kardinali Bergoglio hazina msingi wowote!
Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, kampeni za kutaka
kumchafua Kardinali Jorge Mario Bergoglio, ambaye kwa sasa ni Baba Mtakatifu Francis,
zimechapishwa na gazeti moja ambalo linajipambanua kwa kampeni chafu za kutaka kuwapaka
watu matope. Ni gazeti ambalo limekuwa likiendesha kampeni dhidi ya Makleri, kiasi
kwamba, si jambo la kushangaza kusikia gazeti hili limeibuka kwa mara nyingine tena
kutaka kumchafua Kardinali Bergoglio.
Shutuma zinazotolewa na gazeti hili zinapata
chimbuko lake, wakati Bergoglio alipokuwa nchini Argentina kama Mkuu wa Shirika la
Wayesuit, pale ambapo Mapadre wawili walipotekwa nyara na kwamba, hakuweza kutoa kinga
dhidi ya Mapadre hao wasitekwe nyara.
Padre Lombardi anafafanua kwamba, shutuma
hizi hazina msingi wowote. Vyombo vya sheria nchini Argentina wakati fulani vilimhoji
kuhusu shutuma hizi, lakini hakuna hata siku moja vilipomkuta na hatia wala shitaka
la kujibu. Mhusika mwenyewe alikana shutuma hizi na kuhifadhiwa.
Padre Lombardi
anabainisha kwamba, kuna vielelezo na ushahidi mkubwa kutoka kwa watu mbali mbali
wanaonesha kwamba, Bergoglio aliwalinda na kuwapatia hifadhi wakati wa madhulumu nchini
Argentina, pale nchi ilipokuwa inatawaliwa kwa mtutu wa bunduki.
Mchango wa
Bergoglio unafahamika sana, pale alipoteuliwa kuwa Askofu, alipoanzisha mchakato wa
kuomba msamaha kwa ajili ya Kanisa la Argentina kwamba, wakati wa madhulumu, Kanisa
Katoliki halikujishughulisha sana kuwalinda na kuwatetea wanyonge na wote waliokuwa
wanadhulumiwa na utawala wa Kidikteta.
Shutuma hizi zinafumbatwa katika upembuzi
yakinifu wa masuala ya kihistoria na kijamii wakati wa utawala wa kidikteta, zilizofanywa
na makundi dhidi ya Makleri, kama njia ya kulishambulia Kanisa. Shutuma zote hizi
hazina msingi na lazima zipingwe kwa kauli moja. Ndivyo Padre Federico Lombardi, Msemaji
mkuu wa Vatican anavyohitimisha maneno yake dhidi ya shutuma zinazolenga kumpaka matope
Kardinali Bergoglio.