Ratiba elekezi ya Papa Francis kuanzia tarehe 17 hadi 24 Machi 2013
Ifuatayo ni Ratiba Elekezi ya shughuli muhimu zinazotarajiwa kutekelezwa na Baba Mtakatifu
Francis kuanzia Jumapili tarehe 17 hadi tarehe 24 Machi 2013. Jumapili tarehe 17 Machi
2013, saa 4:00 asubuhi, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia
ya Mtakatifu Anna, iliyoko ndani ya Mji wa Vatican. Baadaye, atasali Sala ya Malaika
wa Bwana na waamini, mahujaji na watalii watakaokuwa wamefika kwenye Uwanja wa Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, majira ya saa 6:00 mchana kwa saa za Ulaya.
Jumatatu,
tarehe 18 Machi 2013, saa 6:50 mchana anatarajiwa kukutana na Rais wa Argentina kwenye
Makao yake ya muda yaliyoko Domus Sanctae Marthae.
Jumanne, tarehe 19 Machi
2013, saa 3:30 asubuhi ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, mwanzo wa utumishi wake
kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Atapata pia nafasi ya kuzungumza na wawakilishi wa
Serikali watakaohudhuria tukio hili la kihistoria na baadaye, atapata chakula cha
mchana na wageni waalikwa kule Domus Sanctae Marthae.
Jumatano tarehe 20 Machi
2013 kwenye Ukumbi wa Clementina, atazungumza na viongozi wawakilishi wa madhehebu
na dini mbali mbali, kama kielelezo cha mshikamano wa udugu katika kuwahudumia watu,
kwa pamoja wakipania kujenga umoja na udugu, kwa ajili ya mafao ya wengi.
Ijumaa,
tarehe 22 Machi 2013 Baba Mtakatifu Francis atakutana na kuzungumza na Mabalozi na
Wawakilishi wa nchi na Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican.
Jumamosi, tarehe
23 Machi 2013 ataondoka kwa Elkopta kuelekea Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo ili kukutana
na kuzungumza na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita na huko watapata
chakula cha pamoja na baadaye atarudi Vatican.
Jumapili, tarehe 24 Machi 2013,
Jumapili ya Matawi na Siku ya Vijana Kijimbo, Baba Mtakatifu Francis kwa mara ya kwanza,
ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
na baadaye kusali Sala ya Malaika wa Bwana.