Papa amtembelea Kardinali Jorge Mejia Hospitalini; wengi wapigwa na butwaa!
Baba Mtakatifu Francis, Ijumaa jioni, tarehe 15 Machi 2013 amemtembelea Kardinali
Jorge Mejia, mwenye umri wa miaka 90, aliyepatwa ugonjwa wa moyo siku ya Jumatano
tarehe 13 Machi 2013 na kulazimika kulazwa kwenye Hospitali ya Pius XI, iliyoko mjini
Roma. Katika hotuba yake kwa Makardinali siku ya Alhamis, aligusia hali ya Kardinali
Mejia na kusema kwamba, inaendelea vyema na alikuwa anawatakia matashi mema katika
maisha na utume wao.
Kardinali Mejia alizaliwa Jimbo kuu la Buenos Aires na
kwa miaka kadhaa alifanya utume wake mjini Vatican kama Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa
la Maaskofu. Alikuwa Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki yenye utajiri mkubwa
na nyaraka mbali mbali za Kanisa.
Baba Mtakatifu Francis ameifanya ziara hii
inayokwenda sanjari na changamoto alizowapatia Makardinali katika mahubiri yake ya
kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kusema kwamba, hawana budi kutembea, kujenga
na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Wakati wa
ziara yake binafsi Hospitalini hapo, Baba Mtakatifu Francis aliwaomba wafanyakazi
wa Hospitali kusali kwa ajili yake.
Amewashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya
kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na wote wanaoteseka. Alipata nafasi ya kusali pamoja
na baadhi ya watawa wanaohudumia Hospitalini hapo. Baadhi ya wafanyakazi waliposikia
kwamba, Baba Mtakatifu Francis alikuwa Hospitalini hapo, walijitokeza kumlaki, kumsalimia
na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.