2013-03-16 09:01:27

Mwenyezi Mungu amewatembelea tena watu wake!


Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu wa Jimbo kuu la Roma, anamshukuru na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuendelea kuwatembelea watu wake. Kwa namna ya pekee, Kardinali Vallini anamshukuru Mungu kwa kuwaangazia Makardinali kiasi hata cha kumchagua Papa Francis kuwa mchungaji mkuu wa Kanisa Katoliki. Jimbo kuu la Roma, linayo furaha isiyokuwa na kifani kumpokea Askofu wake mkuu, atakayewaongoza waamini katika hija ya kweli za Kiinjili kwa sasa na kwa siku za usoni.

Kardinali Vallini anasema, amekwishaonesha utii wake kwa Baba Mtakatifu Francis tangu siku ile alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Amefanya hivi pia kwa niaba ya Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Roma. Kanisa Jimboni Roma, litaendelea kuwa karibu zaidi na Askofu wake mkuu, kwa njia ya imani na unyenyekevu, ili Papa Francis aweze kutekeleza dhamana na utume wake kwa ufanisi, weledi na tija mintarafu mwanga wa Injili.

Kanisa katika kipindi cha siku chache zilizopita, limeshuhudia matukio ambayo yamelitikisa, kiasi kwamba, hata waamini wakatikisika kwa uchungu, waliposikia kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa utashi na uhuru kamili alikuwa amemua kung’atuka madarakani, tukio ambalo limeshuhudiwa na mamillioni ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, siku ile ya tarehe 28 Februari 2013. Imekuwa ni fursa ya kusafisha na kuimarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwatembelea watu wake kwa mifano hai ya ushuhuda wa maisha!

Makardinali katika mkutano wao elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hali wakiwa wameungana katika mshikamano wa upendo na umoja; ukweli na uwazi; wamelichambua Kanisa kama “njugu mawe”; wakabainisha mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji wa maisha na utume wake; fursa zilizopo na changamoto kwa siku za usoni kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Makardinali wameonesha ujasiri na imani thabiti, wakadhamiria kusimama kidete, kutembea kifua mbele kutangaza kweli za Kiinjili, hadi miisho ya dunia. Wamedhamiria kupambana na utepetevu wa imani na mmong’onyoko wa kimaadili, ili kuwajengea tena waamini ile imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake.

Kanisa linaendelea kuwachangamotisha waamini katika ujumla wao, kuonesha ushuhuda makini wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kurithisha imani hii kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kuwahudumia na kuwajali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa ni hai na linaendelea kung’ara na kushamiri kutokana na utakatifu wake, licha ya madoa ya dhambi yanayooneshwa wakati mwingine na watoto wake, lakini wote wako katika hija ya kujitakatifuza mintarafu changamoto iliyotolewa na Kristo mwenyewe! Kuna waamini ambao wanaendelea kujipambanua kutokana na utakatifu wa maisha. Kumbe, hakuna haja ya kukata tamaa, anasema Kardinali Agostino Vallini.

Anawashukuru waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliounganisha sala yao kwa ajili ya kuombea mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakasubiri kwa imani na matumaini, hadi pale moshi mweupe pe! Ulipotoka, kengele zikagonjwa, watu wakafurahia kusikia kwamba, Kanisa limempata Kiongozi mkuu naye ni Baba Mtakatifu Francis. Huyu kwa hakika amekuwa ni sala ya wengi, kiongozi ambaye anajitoa kimaso maso kwa ajili ya kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu!

Amechaguliwa ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani na matumaini, ili waweze kusimama kidete kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni la wote: watakatifu na wadhambi wanaojitahidi kujisafisha kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na matendo ya huruma ili waweze kuiona ile njia ya uzima wa milele. Maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi, wataonja upendo wa kibaba! Jina Francis ni moto wa kuotea mbali!

Ni kauli mbiu inayotamulisha utume na dhamana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sasa na kwa siku za usoni. Roma haina budi kuonesha mfano wa upendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa njia utume utakaowezesha imani na upendo kung’ara na kushamiri mioyoni mwa Watu wa Mungu.

Imeandaliwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.