Katika makala haya yanayounga mkono kampeini kali dhidi ya utumwa mambo leo, na tuzamishe
fikira zetu, katika kukitafakai kipindi cha tangu mapambazuko ya Uhuru kwa mataifa
ya Afrika hadi leo hii ambamo mengi ymeadhimisha miaka hamsini ya kuutokomeza ukoloni.
Tukiainisha pia na utekelezaji wa maazimio ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican (Vatican
II) ambao mwaka huu pia tuna sherehekea kutimiza miaka 50 ya uwepo wake, na katika
muono wa Azimio la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Kama ilivyoelezwa
katika dibaji ya hati za Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican, historia ya binadamu,
daima husonga mbele na matukio ya utendaji wake wa kila siku , hadi hatima ya maisha
ya mtu. Ni upigaji wa hatua katika mwendo wa maisha ambamo kwa wafuasi wa Kanisa,
humulikiwa na mwanga mkuu wa Kristu “ binadamu mpya “ mwenye uwezo wa kuwaunganisha
watu wa mataifa yote kuwa familia moja ya Mungu, katika hija hii ya maisha duniani.
.
Baba Mtakatifu Yohane XX111, alipotangaza rasmi Mtaguso huu wa Vatican
II, alisisitiza ulazima wa marekebisho mapya, si kurekebisha kanuni za imani zinazo
dumu milele , ambazo ni mpya kila wakati, ila kutafakari upya upendo uliofumbatwa
katika kweli za imani, uongofu, toba, unyenyekevu na kutangaza kwa nguvu habari njema
ya kukombolewa na upendo wa Injili.
Historia ya Kanisa inatufundisha juu ya
ukuu wa vipaji vya Mungu mwenyewe, ambavyo hufanya kazi ndani ya kanisa, katika
kukabiliana na changamoto na matatizo mengi na ya aina mbalimbali katika harakati
za kutekeleza maazimio yanayotajwa katika hati ya Vatican 11, mojawapo ikiwa azimio
juu ya utume wa walei, katika mazingira ya kijamii.
Mtaguso II unasema, Utume
wa walei katika mazingira ya Kijamii , unadai juhudi za kuipenyeza roho ya Kikristu
ndani ya fikra na desturi , sheria na miundo ya jumuiya wanaoishi kama jukumu na faradhi
ya walei. Katika uwanja huu, walei wanaweza kutimiza utume wa mtu kwa mwenzake aliye
sawa na yeye. Na hivyo wanatimiza ushuhuda wa maisha, si kwa maneno tu lakini kimatendo
katika mazingira ya kazi zao au amali au masomoni au maeneo ya starehe na viburudisho,
na katika mifumo mingine ya maisha.( tz.962).
Walei wanatimiza utume huu
wa Kanisa katika ulimwengu, kwanza kabisa kwa kuambatana na mwenendo wa imani , ambao
kwa njia yake wanakuwa mwanga wa ulimwengu katika kushughulikia yote kwa moyo mnyoofu,
na hivyo wanawavuta wengine kupenda ukweli na wema na hatimaye kulipenda kanisa na
Kristu , kwa mapendo ya kidugu ambayo yanawawezesha kushiriki katika hali za maisha
yote ya kazi, mateso na matumaini ya ndugu zao. Na hivyo inakuwa ni kuiandaa mioyo
ya watu wote polepole, katika utayari wa kutendewa kwa neema inayoweza kuokoa(tz.
963).
Na hivyo nafasi ya utume wa walei kijamii, inapanuka na kuingia kwenye
mipango ya kitaifa na kimataifa , walei kama wahudumu wa hekima za Kristu, katika
kupenda asili ya uadilifu , uaminifu na wajibu wa raia mwema kulingana na haki na
sheria na masharti yote ya Kimaadili na wema wote.
Kwa kukiri heshima
ya asili na haki sawa isiyoweza kuondolewa kwa watu wote wa familia ya binadamu,
inakuwa ni msingi wa uhuru, haki na amani duniani.
Katika misingi hiyo,
turejeshwa katika mada: mapambano dhidi ya utumwa mambo leo ,ambao ni utendaji mbovu
tunaoishi nao, pengine bila kujua lakini upo na ndivyo ilivyo. Kila siku watu wanachukuliwa
na kupelekwa sehemu wasizo zijua kwa ahadi za uongo za kwenda kupata kazi au kuboresha
masilahi yao na kumbe sivyo.
Na inafahamika wazi kwamba, kupuuza na kudharau
haki za binadamu husababisha vitendo vya kishenzi ambavyo huzua vilio na ugandamizaji
dhamiri ya mwanadamu, na matazamio yake ya kuifurahia dunia, kama mtu huru katika
kujieleza na kuikiri imani yake, mtu aliye uhuru dhidi ya hofu na mashaka ya kugandamizwa
na mwingine.
Watu wema, wanajali madhulumu hayo na kuona kwamba, ni wajibu
kutetea na kulinda kisheria upinzani wote dhidi ya dhuluma na uonevu ulio kinyume
na haki za binadamu. Na kuna ulazima wa kukuza hali zote za kujenga urafiki na maridhiano
kati ya watu na mataifa, kama ilivyo tajwa katika hati ya Azimio la Umoja wa Mataifa.
Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wameridhia imani hii katika haki za asili, heshima
na thamani ya binadamu na katika usawa wa haki kwa wanaume na wanawake na kuwa na
nia ya kukuza maendeleo ya kijamii yanayo pania kufanikisha hali bora za maisha kwa
kila binadamu.
Linakuwa ni jambo la lazima, kwa kila mmoja kuwa msharika wa
Umoja wa Mataifa, katika kukuza heshima , haki za binadamu na uhuru wa kimsingi. Uelewe
huu wa pamoja wa haki na uhuru, una umuhimu mkubwa kwa ajili ya utambuzi kamili kwa
ahadi hiyo ya Umoja wa Mataifa.
Hivi karibuni , Askofu Mkuu Giovanni Martinelli,
Mtawala wa Kitume wa Jimbo la Tripoli Libya , akirejea wimbi la ghasia za wababe wa
Kiislamu kushambulia wengine alisema, "katika ukweli wake, ubabe huo, ni matokeo ya
kutojua maana ya uhuru wa mtu. Wengi wao wanadhani mtu kuwa, uhuru ,ni utendaji wa
kiholela usiokuwa na sheria".Hilo pia , matokeo ya kukosa uzoefu wa kuishi katika
hali za uhuru kamili kwamba uhuru daima huandamana na mipaka na kuheshimu wengine.
Ibara ya 1, katika makubaliano ya Umoja wa Mataifa inasema, watu wote wamezaliwa
huru na sawa katika heshima na haki msingi zote za binadamu, na hivyo wanapaswa kutenda
kwa mwelekeo wa roho ya udugu wa mmoja kwa mwingine.
Na Ibara 2 inasema,
kila mmoja ana haki ya kuwa na haki zote na uhuru wote, bila ya ubaguzi wa aina yoyote,
iwe rangi, jinsia, lugha, dini, maoni ya kisiasa au nyingine ya asili ya taifa au
ya kijamii, mali, kizazi ana hali ingine yoyote katika ubindamu wake.
Aidha
azimio linataja kwamba, kila mtu ana haki ya uhuru maisha, na usalama wa mtu. Hivyo
utendaji wowote unaotaka kumlazimisha mwingine kuishi kinyume na matamanio yake au
kumpa vitisho ni kutenda kinyume cha haki za binadamu. Na kwamba, hakuna mtu anayeweza
kufanyishwa kazi katika hali za utumwa au utwana; utumwa na biashara yake yote ni
marufuku katika kila hali. Na hakuna mtu mwenye kuwa na mastahili ya kuteswa
na aina yoyote ya ukatili, unyama au udhalilishaji au adhabu. Na kila mtu, ana haki
ya kutambulika kama mtu mbele ya sheria.
Kwa maana hiyo Ibara ya 7 inasema,
watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki sawa, bila ubaguzi wowote kupata
ulinzi sawa wa sheria. Wote wana haki sawa ya kulindwa dhidi ya ubaguzi na maonevu
yote.
Iwapo ndivyo ilivyo, leo hii ikiwa inapita miaka 50 kwa mataifa mengi
ya Afrika tangu kujipatia uhuru, na kupita kwa miaka karibia mia mbili tangu kutolewa
kwa azimio la kukomesha utumwa na madhulumu yake yote, ni kipindi cha kutosha wana
wa Afrika kuwa na ufahamu wa kutosha juu ya haki hizi. Ndiyo maana inashangaza kuona,
watu bado wanadiriki kunyima wenzao haki msingi katika maisha. Kipindi cha miaka
50 , ni kipindi kinachotazamiwa waliozaliwa wakati huo wa uhuru, sasa wanaingia katika
kundi la watu wazima, waliokomalia katika uhuru , walio elimika na kuuuishi ustaraabu
huu wa uhuru tangu wakiwa watoto.
Katika ukweli wake madhulumu ya kufanyishwa
kazi katika hali ya utumwa inapaswa kuwa simulizi za wakongwe na si za kizazi hiki.
Kwa kuwa madhulumu haya yanatokea katika mazingira yetu tuishimo, je kama
Wakatoliki walei, tunajishughulisha kwa namna gani, kuzuia madhulumu haya , yanayofanywa
na watu wachache werevu wanjanja walaghai, wanaotafuta utajiri kwa kugandamiza wengine?
Bado
akilini mwetu, tunagongwa na matukio yaliyotolewa na vyombo vya habari vya Tanzania
, juu wa watu wanaokwenda bara na kununua watoto na kuwasafirisha hadi Zanzibar kwa
lengo la kuwapeleka mbali zaidi uarabuni na kwingineko, ambako wanatajwa kuishia katika
kazi za sulubu majumbani mwa watu,wakiw wamenyiwa uhuru wao wa kutembea au kupumzika
wanavyotaka.
Haya ni madhulumu makubwa yanayopaswa kukomeshwa mara moja
. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu na hasa vijana , kuhusika na utoaji wa msaada kwa
yeyote anayehisi kuna mtego wa kuuuzwa au kuchukuliwa na watu asiowajua ,na hasa watoto
wa kike na wa kiume pia. Kwa kuzingatia roho ya umoja na ushirikiano inayotajwa na
Kanisa na Azimio la Umoja wa Mataifa, upo mshikamano wa kijamii usioweza kutenguliwa,
wa kila anayezaliwa anakuwa ni sehemu ya jamii. Hivyo jamii inayo haki kamili ya kutaka
maelezo kutoka kwa mzazi, pale mtoto anapotoweka kimya kimya kijijini.
Wazazi
na watu wote wanapaswa kujua kwamba, hali za ajira leo hii si kama ilivyokuwa siku
za nyuma. Kama ilivyo Afrika pia Ulaya na uarabuni, hakuna ajira za kueleweka. Sasa
kama wenyeji wenyewe wanakosa ajira, iweje watoka mbali kwapate ajiri halali kiurahisi
hivyo?
Maisha ni magumu pote duniani . Heri kubaki katika eneo lako la kuzaliwa
ambako kuna mjomba na shangazi wanaoweza kukusaidia ukipatwa na matatizo, kuliko kwenda
majuu asikokujua mtu.
Imeandaliwa nami TJMhella, Idhaa ya Kiswahili ya Redio
Vatican.