CELAM wanamhakikishia Baba Mtakatifu Francis mshikamano wa kidugu katika utekelezaji
wa majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caraibi, katika maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, limemtumia salam na matashi mema Baba Mtakatifu Francis kwa kuchaguliwa
kwake kuliongoza Kanisa Katoliki.
Wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulijalia
Kanisa kiongozi mkuu wa Kanisa ambaye amevuta hisia za wengi tangu wakati wa uchaguzi
wake hadi alipotangazwa hadharani. Yote haya yamefanyika katika kukuza na kudumisha
mshikamano katika shughuli za kichungaji na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maaskofu wa
CELAM wanasema kwamba, kwa hakika, anaonesha zile changamoto za ugunduzi, ari na moyo
wa kimissionari.
Huu ni mwanzo wa hija ndefu kati ya Askofu na Familia ya
Watu wa Mungu Jimboni Roma, Kanisa linalohifadhi kwa namna ya pekee, umoja na upendo.
Ni hija ya udugu, upendo na imani kati yao wote. Ndiyo matashi ya Maaskofu Katoliki
kutoka CELAM.