Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii,
Jumamosi, tarehe 16 Machi 2013 wakati wanahabari walipokutana na Baba Mtakatifu Francis,
aliwatambulisha kwa kusema kwamba, tukio hili lilikuwa limewakutanisha wanahabari
kutoka katika nchi 81 waliofuatilia kwa ukaribu zaidi matukio yaliyokuwa yanatendeka
hapa mjini Vatican, tangu siku ile Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alipong'atuka
kutoka madarakani hadi Baba Mtakatifu Francis alipochaguliwa na kuonekana hadharani.
Kipindi chote hiki, Kanisa Katoliki limekuwa ni mdau mkuu wa vyombo vya habari kutoka
sehemu mbali mbali za dunia.
Wanahabari wamefanya kazi kubwa katika kuwafikishia
watu ujumbe wa kile kilichokuwa kinatendeka hapa mjini Vatican. Ni tukio ambalo watu
wengi wamelifuatilia kwa hisia, mashaka na matumaini. Vyombo vya habari vimetekeleza
wajibu wake kwa uhuru kamili, weledi, busara na hekima kubwa, kwa matukio haya ambayo
ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa. Utofauti wa hadhira inayokusudiwa, mahali
na weledi umeviwezesha vyombo vya habari kufikisha utajiri mkubwa wa maisha na utume
wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.