WCC ina mkaribisha Baba Mtakatifu Francis katika mapambano dhidi ya changamoto za
ulimwengu mamboleo
Dr. Olav Fykse Tvait, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amemtumia salama
za kiekumene Baba Mtakatifu Francis, akimpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza
Kanisa Katoliki, kielelezo kikubwa cha maisha ya Kanisa Katoliki na waamini wa madhehebu
mengine pia.
Baba Mtakatifu Francis ni hujaji wa haki na amani kutoka Amerika
ya Kusini; kiongozi ambaye alijitosa bila ya kujibakiza kutafuta haki jamii, akipania
kuwainua maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kuchaguliwa
kwake ni changamoto ya kuendeleza jitihada za kutafuta haki na amani katika Jumuiya
ya Kimataifa.
Mara baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican,
miaka hamsini iliyopita, Baraza la Makanisa Ulimwengu limeendelea kuwa na uhusiano
na majadiliano ya kina na Kanisa Katoliki katika kutafuta na kujenga umoja wa Kanisa;
ufahamu wa Kanisa, utume sanjari na kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene. Ni
matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, uhusiano mwema kati ya pande hizi
mbili utaendelezwa na kuimarishwa.
Viongozi wa Makanisa wanatambua na kuthamini
mchango wa Baba Mtakatifu Francis katika masuala ya kijamii; majadiliano ya kidini
na kiekumene na kwamba, uzoefu na mang'amuzi yake ya mikakati na shughuli za kichungaji
yatachangia kwa namna ya pekee kabisa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa
Mtakatifu Petro.
Ni matumaini ya Dr. Tveit kwamba, Makanisa yatawajibika
kutoa ushirikiano kwa Baba Mtakatifu Francis, kwa kutambua kwamba, Wakristo wengi
wanaishi katika nchi zinazoendelea duniani. Baba Mtakatifu anakaribishwa na Baraza
la Makanisa Ulimwengu ili kuungana nao katika kupambana na changamoto za dunia.