Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tano ya Kipindi cha Kwaresima
Tunaendelea na tafakari Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha kwaresima mwaka
C, Mama Kanisa ametuwekea Neno ambalo linazidi kusisitiza kuhusu Huruma na Msamaha
wa Mungu kwa walio wakosefu.
Dominika zilizopita
tuliongozwa na Injili ya Mt. Luka na Dominika hii sehemu ya Injili yatoka katika Injili
ya Mt Yohane. Katika sehemu hii ya Injili tunamwona Bwana ambaye anakwenda mlima wa
mizeituni wakati wa usiku, ni katika mpango wa kuunganika na Baba yake aliye mbinguni
kwa njia ya sala.
Kisha maandalizi hayo tunamwona yuko hekaluni akifundisha.
Ghafla akifundisha Mafarisayo na Waandishi wanamleta mbele yake mwanamke aliyefumaniwa
katika uzinzi, wakitaka aadhibiwe vikali kadiri ya torati. Lengo lao ni kumjaribu
Bwana waone anasemaje katika hili ili wapate namna ya kumshitaki. Bwana akijua hila
zao anasema asiye na dhambi awe wa kwanza kumpiga mawe mama huyu. Kila mmoja aliondoka
kwa upole baada ya kusutwa na hali yao ya ndani!
Mpendwa msikilizaji, Mwinjili
anataka tutambue na kumfuasa Bwana ambaye anasali na kung’amua shida za watu. Bwana
atatambua kwanza shida ya mama huyu aliyefumaniwa na ataona hali yake ya ndani na
kisha atakuza moyo wa toba wa mama huyu na kisha atamwambia umesamehewa usitende dhambi
tena. Huu ni wito mkubwa kwetu ambao kila mara tunakuzwa katika moyo wa toba na tunasamehewa
dhambi zetu, tukialikwa kutotenda dhambi tena, na kujikabidhi mikononi mwa Bwana.
Bwana atang’amua shida za Mafarisayo na Waandishi, yaani unafiki wao na kukosa
utambuzi wa kuwa sisi sote tunaihitaji msamaha na huruma ya Mungu. Mwanamke aliyefumaniwa
alibaki na Bwana baada ya wengine kutoweka, hapa Mwinjili ataka kutuambia kuwa katika
shida zote, wengine watakimbia na tutabaki na Mungu anayetupenda katika hali tuliyonayo,
tuwe wadhambi kama mama huyu au wema.
Mpendwa msikilizaji, katika mateso
kama tulivyosema tutabaki na Bwana aliye mwenye upendo na huruma isiyopimika. Jambo
hili tunalipata pia katika somo la I Nabii Isaya anapowaambia Wana wa Israeli akisema
Mungu afanyaye njia katika bahari na kuzima jeshi la adui mfano wa utambi hawezi kuwaacha
kamwe. Anazidi kusema atatenda neno jipya na kufanya njia jangwani na mito ya maji
nyikani.
Kwa hakika Nabii Isaya yuko katika maono anaona jinsi Mungu anavyowatoa
katika utumwa wao huko Babeli. Anawafundisha Waisraeli wasiyakumbuke mambo ya zamani
bali fadhila na zawadi anazowapa kwa sasa yaani uhuru kamili. Anawakumbusha jinsi
Mungu alivyowatoa katika utumwa huko Misri ndivyo ambavyo upendo wake bado ulivyo
na hautakuwa na mwisho.
Mtume Paulo anapowaandikia Wafilipi anawafundisha kumtazama
Kristu aliye chanzo na mwisho wa maisha yao. Mtume Paulo akitaka kukazia ukuu wa Bwana,
anasema kwake yeye mambo yote ya kidunia ni hasara isipokuwa kumjua Kristu. Anakuja
na lugha kali kidogo akisema mambo yote ni kama kinyesi isipokuwa kumjua Kristu.
Hata
hivyo anaacha nafasi ya unyenyekevu akisema si kwamba nimekwishakuwa mkamilifu bali
bado nakaza mwendo ili nilipate lile ambalo kwalo nimeshikwa na Kristu. Huu ni ushuhuda
wa hali ya juu wa kukiri Neno la Mungu kwa umahiri na umakini wa hali ya juu. Mkristo
wewe, unapaswa kuwa ushuhuda mbele ya mataifa kama Mtume Paulo. Hata hivyo ni ngumu
kumbe unahitaji kuwa na moyo mchanga ambao haujaharibiwa na chafuzi za dunia, ili
uweze kupokea mambo mapya ya Kikristo.
Mpendwa mwana wa Mungu, Yesu Kristo
ndiye mfano wetu hai na ndiye taa ya kutuongoza. Mtume Paulo anatoka katika hali ya
ufarisayo anauchuchumalia ukristu kwa neema ya Mungu kwa ushujaa. Kuwa mkristu kunadai
kujinasua kwa namna ya pekee tena ya juu, kuacha tamaduni fulanifulani ambazo zaweza
kuzuia mapenzi ya Mungu.
Tunaalikwa katika Dominika hii kuwa makini kuepuka
kushabikia makosa ya wengine, kuacha kutazama wengine katika mlengo wa fitina bali
mlengo wa upendo ambao husamehe daima hata kama dhambi yatisha kama nini! Basi mpendwa
nikutakie Kwaresima njema iliyojaa toba na msamaha daima. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.