2013-03-15 14:29:34

Mshikamano na upendo katika kumshuhudia Kristo na Kanisa lake!


Baba Mtakatifu Francis, Ijumaa, tarehe 15 Machi 2013 amekutana na kuzungumza na Makardinali kwa kuwashukuru kwa moyo wa upendo na mshikamano. Hiki kimekuwa ni kipindi ambacho watu wengi wamefuatilia kwa moyo mkuu matukio mbali mbali yaliyokuwa yanafanyika hapa mjini Vatican, hata kama walikuwa ni watu wenye imani tofauti.

Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamemsindikiza kwa njia ya sala Khalifa wa Mtakatifu Petro. Umati mkubwa wa watu uliokuwa umekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, umeacha picha ya kudumu katika moyo wake. Anawashukuru wote kwa uwapo wao katika maisha yake ya kiroho.

Baba Mtakatifu Francis amewashukuru viongozi waandamizi waliokuwa wanaangalia maisha na utume wa Kanisa wakati ambapo Kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kilipokuwa wazi. Amewakumbuka Makardinali ambao kutokana na umri na hali yao ya afya hawakuweza kushiriki katika mikutano ya Makardinali, lakini wameendelea kulitumikia Kanisa kwa njia ya mateso na sala zao. Anawashukuru wote waliohusika katika kuandaa na hatimaye, maadhimisho ya Conclave.

Amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliyeliongoza Kanisa kwa imani, unyenyekevu na hekima kubwa, mambo ambayo yanaendelea kuwa ni sehemu ya urithi wa maisha ya kiroho kwa Kanisa zima. Papa Benedikto wa kumi na sita ni kiongozi aliyekuwa na upendo mkubwa kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka; Kristo ambaye ni hai katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu Francis anawaalika Makardinali kuendelea kumsindikiza Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa njia ya sala. Uwepo wake bado unaendelea kusikika ndani ya Kanisa kwa njia ya sala na tafakari zake za kina, ili kulisindikiza Kanisa katika hija ya maisha yake ya kiroho na kimissionari.

Mkutano kati ya Papa na Makardinali ni mwendelezo wa moyo wa umoja, upendo na mshikamano waliouonesha wakati wote wa uchaguzi, huku wakisukumwa na upendo kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi kwamba, waliweza kushirikishana: mawazo, mang'amuzi na uzoefu wao, kiasi kwamba, kwa sasa wengi wao wanafahamiana zaidi na hivyo kujenga Jumuiya inayosimikwa katika urafiki kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kushirikiana na Roho Mtakatifu mdau mkuu katika maisha na utume wa Kanisa.

Anasema, Roho Mtakatifu ndiye kiini cha umoja unaojionesha hata katika tofauti msingi za karama na vipaji, lakini yote haya ni kwa mafao ya Kanisa linaloabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francis anasema kwamba, kwa mshikamano wa dhati na Makardinali, anajisikia ile dhamana na ari ya kulitumikia Kanisa, ili liendelee na Kristo na ndani ya Kristo, kwa kujikita zaidi na zaidi katika kuimarisha Imani katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Waamini wajitahidi kumpeleka Kristo kwa watu na watu wajitahidi kumwendea Kristo aliye njia, ukweli na uzima na hai ndani ya Kanisa lake. Anayebahatika kukutana na Kristo kwa njia ya Kristo anapata neema na baraka za kufurahia maisha yake ya Kikristo.

Kristo anaendelea kuliongoza Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu, ili wote kwa pamoja waweze kushikamana, kujenga na kuliimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, bila ya kukata tamaa na kumwachia shetani kulitawala. Ni changamoto ya kuendelea kumsikiliza Roho Mtakatifu anayelikirimia Kanisa mbinu mpya za Uinjilishaji, hadi miisho ya dunia, kwa kusikiliza kilio na shida za watu, dhamana endelevu ya kazi za kimissionari.

Baba Mtakatifu Francis anasema uzee ni kikao cha hekima na maisha yanayomwezesha mwamini kumfahamu Yesu Kristo, zawadi inayopaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya; ni kipindi cha utulivu na sala. Huu ni utajiri ambao Kanisa halina budi kuwashirikisha vijana sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francis anauweka utume na maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro chini ya ulinzi na maombezi ya Bikira Maria, ili aweze kuwaongoza waamini katika hija ya maisha, wakisikiliza kwa makini sauti ya Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.