2013-03-15 09:31:35

Changamkieni masomo, dunia leo hii ni tambara bovu!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuachana na siasa na uhanarakati na kuelekeza nguvu yao kwenye masomo kwa sababu hayo ni mambo yanayowapoteza muda wa masomo na kuwa suala la kufaulu ama kufeli ni suala binafsi na wala halina ubia na mtu mwingine.
“Nawasihi mjiepushe na mambo yanayowapungumzia muda ama kuwaondoa katika shughuli ya msingi iliyowaleta hapa ya kujifunza, ili mpate digrii katika fani mliyochagua wenyewe kuisomea. Vishawishi ni vingi na watu wanaopanga kuwashawishi ni wengi lakini lazima mkumbuke lililowaleta chuoni,” Rais Kikwete amesema hayo, Alhamisi, Machi 14, 2013, mjini Morogoro.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na wana Jumuiya ya Chuo Kikuu na wananchi walioko jirani na chuo hicho baada ya kuweka jiwe la msingi katika Jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na kufungua rasmi Jengo la Kitivo cha Sayansi kwenye Chuo Kikuu cha Waislamu cha Mororgoro (MUM) kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro.
Rais amewaambia wanajumuiya hiyo: “Mwanafunzi wa Chuo Kikuu ni mtu mzima. Si mtoto. Lazima mjue kuwa mnawajibika kwa kila unaloliamua na kulitenda. Amua kuwajibika vizuri. Fikiri kabla ya kutenda. Changanua lipi la kufanya. Wakati wote uongozwe na busara na hekima na siyo na jazba au ushabiki na matakwa ya kundi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kama ni jema fanya na kama siyo jema usifanye. Lazima ujue kuwa hatma ya yote uko peke yako. Katika masomo unanufaika wewe. Utafaulu ama kufeli wewe. Utapata shahada wewe na siyo mtu mwingine. Hakuna ubia wa kufaulu ama kufeli ama kiwango cha kufaulu.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Shirikiana na wengi lakini usisahau kujali maslahi yako. Mengi ya wengi yasiyojumuisha yako yahoji vizuri kabla ya kuamua kushiriki au kufanya. Vinginevyo labda kama umeamua kujitoa muhanga, uwe shujaa. Hata kwa hilo,sijui utakuwa shujaa na nani? Kama unaamua kuwa shujaa kwa kushiriki siasa na uhanarakati, shauri yako.”
Mapema, Rais Kikwete aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa awamu ya kwanza ya Jengo la ICT na pia kuzindua rasmi Jengo la Kitivo cha Sayansi kwenye Chuo Kikuu hicho ambacho ni moja ya vyuo vya juu 68 nchini.
Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Hamza Mustafa Njozi amemwambia Rais Kikwete kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Jengo la ICT mpaka sasa imegharimi kiasi cha dola za Marekani 350,000, sawa na asilimia 16 ya gharama zote za ujenzi, ambazo zimetolewa kama msaada na Benki ya Maendeleo ya Kiislam ya Islamic Development Bank (IDB) yenye makao yake Saudi Arabia.
Profesa Njozi amesema kuwa jengo la Kitivo cha Sayansi limegharimu sh milioni 450 na wanafunzi wapatao 500 wananufaika na kujengwa kwa jengo hilo jipya. Kundi la kwanza la wananchi hao lilimaliza masomo yao Novemba, mwaka jana, 2012.
MUM ambacho kinaendeshwa na taasisi ya mfuko wa Kiislamu iitwayo Muslim Development Fund (MDF) kilianzishwa kutoa masomo mwaka 2005 baada ya Rais Benjamin Mkapa kutoa majengo yaliyokuwa ya Chuo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa MDF kwa madhumuni ya kuanzisha chuo hicho kikuu cha kwanza kuendeshwa na Waislam nchini.
Idadi ya wanafunzi wa chuo hicho imeongezeka kutoka 167 miaka saba iliyopita katika mwaka wa kwanza wa 2005 hadi kufikia 2,678 wa sasa ambao kati yao 1,571 ni wanaume. Kwa sasa chuo hicho kina wahadhiri wa kudumu 45 na wahadhiri wa muda 50.
JK: Tulipanua elimu kwa sababu tulikuwa nyuma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake iliamua kupanua kwa kiwango kikubwa elimu nchini kwa ngazi zote kwa sababu Tanzania ilikuwa nyuma sana ya nchi nyingine jirani katika sekta ya elimu miaka saba iliyopita.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake ilichukua uamuzi huo wa busara kwa sababu vijana wengi wa Tanzania waliostahili kupata elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwa hawaipati elimu hiyo.
Rais Kikwete ameyasema hayo, Alhamisi, Machi 14, 2013, wakati alipohutubia wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) na wananchi wanaoishi jirani na chuo hicho baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa Jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na kufungua Jengo la Kitivo cha Sayansi kwenye chuo hicho kwenye eneo la Msamvu, mjini Morogoro.
Rais Kikwete amewaambia wananchi hao: “Katika Kipindi cha miaka saba, Serikali yetu imeongeza sana uwekezaji katika upanuzi wa elimu tangu ya awali hadi elimu ya juu. Tuliamua kufanya hivyo kwa sababu vijana wengi waliokuwa wanastahili kupata elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwa hawaipati.”
Ameongeza: “Tanzania ni kubwa mara mbili kuliko Kenya na mara tatu kuliko Uganda kwa eneo na idadi ya watu lakini sisi ndiyo tulikuwa na idadi ndogo zaidi ya wanafunzi katika ngazi hizo zote. Kwa mfano, mwaka 2005, idadi ya wanafunzi waliokuwa Chuo Kikuu nchini Kenya ilikuwa 108, 407, Uganda 88,360, na baadhi ya nchi za SADC kama vile Afrika Kusini idadi hiyo ilikuwa 717, 973. Wakati wenzetu walikuwa na idadi hiyo, sisi tulikuwa na wanafunzi 40, 719 tu katika vyuo vikuu nchini.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “ Hali hiyo ilikuwa pia kwa elimu ya sekondari. Kenya ilikuwa na wanafunzi 925,341, Uganda 619,519 na Afrika Kusini 4,186,882 wakati Tanzania ilikuwa na wanafunzi 524,325 tu waliokuwa katika shule za sekondari. Hali hii haikukubalika na tukaamua hatuwezi kuiachia iendelee. Tukachukua hatua tulizozichukua.”
Rais Kikwete amesema kuwa matokeo ya uamuzi ni kwamba vijana wengi wa Tanzania leo wanapata fursa kubwa zaidi za elimu kuliko wakati wowote katika “historia ya nchi yetu.” Amesema kuwa sasa kazi inayoendelea ni kuimarisha ubora wa elimu wapatayo vijana wa Tanzania kwa kuongeza idadi ya walimu, vifaa vya kufundishia na vitabu.
Ameongeza Rais Kikwete: “Kufuatia juhudi hizo, idadi ya wanafunzi waliopo kwenye vyuo vikuu nchini imeongezeka sana, kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi kufikia 166,484 mwaka 2012. Kwa upande wa sekondari mwaka 2011 tulikuwa na wanafunzi milioni 1.79 na wenzetu wa Kenya walikuwa na wanafunzi 1.77. Haya ni mafanikio makubwa na Serikali itaendelea kuwekeza katika upanuzi wa fursa za elimu na ubora wake.”
Rais Kikwete pia amesifu, kupongeza na kuwashukuru wadau wengine wa elimu ambao wametoa mchango mkubwa katika kupanua fursa ya elimu kwa vijana wa Tanzania. “Kwa mfano, katika vyuo vikuu 49 vilivyopo nchini kwa sasa, vinavyomilikiwa na umma ni 14 tu. Vyuo vikuu 24 vinamilikiwa na mashirika ya dini na 11 ni vya sekta binafsi.”








All the contents on this site are copyrighted ©.