Ifuatayo ni ratiba elekezi ya Baba Mtakatifu Francis anapoanza utume wake kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro. Tarehe 14 Machi 2013, Baba Mtakatifu asubuhi anatembelea kwenye
Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu. Hii ni hija binafsi ya kiroho kwa heshima ya Bikira
Maria Mama wa Mungu na Kanisa.Alipofika kanisani hapo, alisali kwa kitambo kidogo
na baadaye akaondoka, akiwa ameandamana na baadhi ya viongozi waandamizi wa nyumba
ya kipapa.
Alhamisi, tarehe 14 Machi 2013, Majira ya jioni saa 11:00 Jioni
kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francis ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Makardinali
walioshiriki kwenye uchaguzi wa Papa Mpya. Ibada hii inaadhimishwa kwenye Kikanisa
cha Sistina, mahali ambapo Makardinali walikuwa wanafanyia uchaguzi.
Ijumaa,
tarehe 15 Machi 2013, Majira ya saa 5:00 asubuhi, Baba Mtakatifu Francis atakutana
na kuzungumza na Makardinali wote.
Jumamosi tarehe 16 Machi 2013 Baba Mtakatifu
atakutana na kuzungumza na Waandishi wa Habari kutoka sehemu mbali mbali za dunia
ambao wako hapa mjini Vatican kuhabarisha ulimwengu yale yanayojiri wakati huu pamoja
na kuwashukuru kwa kazi kubwa waliyoifanya. Mkutano huu na wanahabari utafanyika kwenye
ukumbi wa Paulo wa sita, hapa mjini Vatican.
Jumapili, tarehe 17 Machi 2013,
Baba Mtakatifu Francis, kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, atasali
na waamini, mahujaji na wageni watakaofika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican Sala ya Malaika wa Bwana.
Jumanne, tarehe 19 Machi 2013,
Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu, Papa Francis ataadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hapa utakuwa
ni mwanzo rasmi wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika Ibada hii ya
Misa Takatifu Makardinali watarudia kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ibada hii inatarajiwa kuanza saa 3:30 kwa saa za Ulaya.
Jumatano tarehe 20
Machi 2013, Baba Mtakatifu Francis, atakutana na kuzungumza na wawakilishi kutoka
sehemu mbali mbali za dunia watakaokuwa wamefika hapa mjini Vatican kwa ajili ya tukio
hili. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Jumatano ijayo, hakutakuwa na Katekesi ambayo
kwa kawaida inatolewa na Baba Mtakatifu kila siku ya Jumatano.
Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican itaendelea kuwa nawe bega kwa bega katika matukio yote haya!