Papa Francis anawashukuru na kuwaomba waamini kusali kwa ajili yake na Kanisa!
Bahari ya waamini, mahujaji na watalii ilifurika Jumatano Usiku, wakati waliposikia
kengele za Kanisa kuu la Mtakatifu Petro zikipigwa na moshi mweupe ukiendelea kutoka
kwenye paa la Kikanisa cha Sistina, ishara kwamba, Kanisa limempata Khalifa wa Mtakatifu
Petro, ambaye tangu sasa anajulikana kama Francis
Wakati akitoa
baraka zake za kichungaji kwa mji wa Roma na Dunia kwa ujumla, "Urbi et Orbi" alisema
kwamba, Makardinali katika mkutano wao wa uchaguzi wamefunga safari ndefu hadi miisho
ya dunia ili kuwapatia Askofu wa Roma. Kwanza kabla ya yote, aliomba sala kutoka kwa
waamini na kila mtu mahali alipokuwa alisimama kwa kitambo kidogo ili kusali na kumwombea
Baba Mtakatifu Francis.
Amewashukuru kwa makaribisho ya nguvu na kwa namna
ya pekee, aliwaomba waamini na mahujaji waliokuwa wamemiminika kwenye Uwanja wa Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro pamoja na viunga vyake, kusali kwa ajili ya kumwombea Papa
mstaafu Benedikto wa kumi na sita.
Baada ya sala hii, Baba Mtakatifu Francis,
aliwaambia waamini kwamba, kwa sasa wakiwa wanaandamana na Askofu wao, wanaanza hija
ya Kanisa la Roma ambalo ni kielelezo cha upendo kwa Makanisa yote. Hii ni hija ya
mshikamano wa kidugu na imani miongoni mwa watu wa Familia ya Mungu. Amewashukuru
viongozi mbali mbali wa Kanisa watakoshirikiana naye katika mwendelezo wa mchakato
wa Uinjilishaji mpya, kwa Mji wa Roma.
Kwa mara nyingine Baba Mtakatifu Francis
aliomba sala kwa waamini waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro na baadaye akatoa baraka ya kitume "Urbi et Orbi".