2013-03-14 10:22:54

Baba Mtakatifu Francis ni kiongozi anayetaka kutoa huduma kwa Kanisa la Kristo!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Kanisa limempokea kwa mikono miwili, Baba Mtakatifu Francis anayetoka Amerika ya Kusini ambako kwa sasa Kanisa lina waamini wengi wenye fursa na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa.

Uchaguzi wa Jina la Francis una maana kubwa katika maisha na utume wa Papa Francis, jina amblo kwa mara ya kwanza linatumika katika historia ya Kanisa kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni jina linalobainisha unyofu na ushuhuda wa Kiinjili, mambo ambayo yamejionesha kwa Baba Mtakatifu alipotokeza hadharani kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hapo Jumatano tarehe 13 Machi 2013.

Ameonesha unyenyekevu wa hali ya juu kwa kuomba sala na baraka kutoka kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kabla hata ya Yeye mwenyewe kuwapatia baraka yake ya kitume! Ni mtu wa sala, kama ilivyojionesha pia wakati akizungumza na waamini wa Jimbo kuu la Roma. Inapendeza kuona Familia ya Mungu inasali kwa pamoja.

Baba Mtakatifu Francis ni Myesuit na Wayesuit wanajipambanua na Watawa wa Mashirika mengine kwa njia ya huduma kwa Kanisa, kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Uongozi ni huduma na wala si uchu wa madaraka!

Huu ndio mwelekeo unaoneshwa na Kanisa kwa wakati huu kwamba, watu wanaalikwa kuhudumia na kwamba Baba Mtakatifu Francis ni mtu anayeonesha kwamba, kweli anataka kulihudumia Kanisa, kwani uchaguzi wake umekuja wakati ambapo Papa Benedikto wa kumi na sita, alipoamua kung'atuka madarakani, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma kwa Mungu na jirani, kwa kutambua uwezo na umri wake.

Baba Mtakatifu Francis amezungumza tayari kwa njia ya simu na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita na kwamba, anaendelea kumwombea katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.







All the contents on this site are copyrighted ©.