2013-03-13 08:03:50

Waamini nchini Rwanda wanasali kwa ajili ya uchaguzi wa Papa Mpya


Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea ufanisi katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unaoendelea kwenye Kikanisa cha Sistina mjini Vatican. Hayo yamo kwenye taarifa ya mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda uliohitimishwa hivi karibuni chini ya uongozi wa Askofu Smaradge Mbonyitenge, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda.

Pamoja na mambo mengine, Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda limeipembua bajeti ya mwaka 2012 pamoja na kupitisha bajeti kwa ajili ya mwaka 2013. Maaskofu wanaridhika na hatua ya udhibiti wa fedha na mali ya Kanisa, kwa kuzingatia tija, weledi, ukweli na uwazi, kwa kutambua kwamba, fedha na mali ya Kanisa ni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za kitume. Maaskofu pia wamesomewa taarifa ya Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Rwanda, Caritas Rwanda linaloshirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Maaskofu wanaendelea kuhimiza ushirikiano baina ya pande hizi mbili kwa ajili ya kukoleza maboresho katika huduma ya afya, elimu na maendeleo endelevu nchini Rwanda.

Idara ya Katekesi imeelezea mikakati inayoendelezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda katika ufundishaji wa elimu ya dini shuleni na katekesi kwa wakatekumeni Maparokiani. Maaskofu wanasema, kuna mapungufu makubwa yaliyojitokeza katika ufundishaji wa Katekesi kwa Wakatekumeni, suala ambalo litapembuliwa kwa kina na mapana wakati wa Mkutano wa Baraza la Maaskofu Rwanda, mwezi Mei, 2013. Tarehe 20 Machi Maaskofu watakutana tena kufanya tathmini ya kina kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.







All the contents on this site are copyrighted ©.