Makardinali 115 wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura, Jumatano, tarehe 13 Machi
2013, baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waliingia kwenye Kikanisa
cha Sistina kwa ajili ya kusali masifu ya asubuhi na baadaye wakaendelea na mchakato
wa kupiga kura.
Leo Makardinali wanatarajia kupiga kura mbili asubuhi na mbili
jioni. Wakati wote huu, macho na masikio ya waamini na watu wenye mapenzi mema yanaendelea
kuelekezwa kwenye Paa la Kikanisa cha Sistina, kitakachotoa alama ya moshi mweupe
alama ya kwamba Kanisa limempata Papa Mpya; moshi mweusi, alama kwamba, mchakato bado
unaendelea!
Waamini wanakumbushwa kwamba, uchaguzi wa Papa ni tofauti kabisa
na uchaguzi unaofanywa katika medani za kisiasa au katika uchaguzi wa mkurugenzi mkuu
wa Shirika la Kimataifa. Hapa Makardinali wamekusanyika kwa ajili ya kumchagua Kiongozi
wa Kanisa, atakayepewa dhamana ya kuongoza Jumuiya ya Waamini. Kumbe, yule atakeyechaguliwa
kwanza kabisa hana budi kuwa na sifa njema za maisha ya kiroho: mchamungu, anayejitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili kutangaza kweli za Kiinjili, mtu anayeaminika na kukubalika
na Kanisa na Jamii ya watu wanaomzunguka.
Conclave ni kipindi maalum cha imani,
matumaini, mapendo na mshikamano miongoni mwa Makardinali na Kanisa kwa ujumla, ndiyo
maana Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kuwasindikiza Makardinali
katika sala. Conclave ni tukio la Liturujia ya Kanisa inayoadhimishwa kwenye Kikanisa
cha Sistina, chenye utajiri mkubwa wa sanaa, kinachotoa fursa kwa Makardinali: kusali
na kutafakari maajabu na ukuu wa Mungu, wakitambua dhamana waliyokabidhiwa na Kanisa
ya kuchagua Kiongozi mkuu.
Hapa hakuna mgawanyiko kama baadhi ya wanahabari
wanavyotaka kuwaaminisha wasomaji, watazamaji na wasikilizaji wao! Katika mikutano
elekezi, Makardinali wamezungumza katika ukweli na uwazi; mwanga wa Kanisa na Vivuli
vinavyoliandama Kanisa; yote haya yamefanyika katika matumaini, utulivu wa ndani na
uhuru kamili. Makardinali wakikamilisha mchakato wa uchaguzi, ulimwengu utafahaamishwa
mara moja!
Itakumbukwa kwamba, kila siku, Makardinali kadiri ya Misale ya Conclave,
wanaweza kuchagua nia ya misa moja kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa: kwanza kabisa
kwa kufuata liturujia ya siku; kumwomba Roho Mtakatifu; kusali kwa ajili ya Kanisa
zima; kumwomba Bikira Maria au kusali kwa ajili ya maombezi ya Watakatifu Petro na
Paulo.