Mikakati ya kuimarisha tunu bora za maisha na wito wa familia ndani ya Kanisa na Jamii
kwa ujumla!
Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia, hivi karibuni alizundua
matarajio ya Baraza la Kipapa la Familia baada ya Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa
yaliyofanyika Jimbo kuu la Milano, Mei 2012.
Tukio hili ambalo lilikusanya
Familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lilidhihirisha umuhimu wa Familia katika
Jamii na Kanisa, licha ya matatizo na magumu ambayo familia nyingi zinaendelea kukumbana
nayo katika maisha na utume wake kwenye ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi
na teknolojia.
Lakini bado familia inabaki kuwa ni rasilimali kuu katika Jamii,
kama tafiti nyingi zinavyobainisha kwamba, hapa ni mahali ambapo watu wengi wanapenda
kukimbilia kwa ajili ya kupata faraja, amani na utulivu na kwamba, familia ni tarajio
la vijana wengi ambao pia wameonesha kwamba, wanapenda kuishi katika ndoa kadiri ya
Mafundisho ya Kanisa.
Huu ni ukweli unaoibuliwa kutoka katika undani wa mwanadamu,
jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na shinikizo linalooneshwa na baadhi ya watu
kutaka kushabikia vitendo vinavyokwenda kinyume cha utu na maadili mema; hawa ni wale
wanaotaka kufunga ndoa za watu wa jinsia moja, jambo ambalo linaonekana kuwa ni fashion
kwa nchi nyingi za Ulaya. Ubinafsi ni kati ya vikwazo vinavyoendelea kudumaza tunu
msingi na maisha yakifamilia.
Jambo la pili anasema Askofu mkuu Paglia ni
watu kutaka uhuru usiokuwa na mipaka; uhuru usiozingatia maadili na utu wema; ni uhuru
ambao kimsingi hautaki kuwajibika. Lakini ikumbukwe kwamba, familia ni taasisi inayowajibisha
na kufungamanisha watu katika kifungu cha upendo mkamilifu. Madhara ya utandawazi
yanapelekea baadhi ya watu kujitafuta wenyewe kiasi kwamba, hawana tena habari za
kutaka kuishi pamoja kama Bwana na Bibi kadiri ya mpango wa Mungu sanjari na kulea
watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kanisa linaendelea kusimama
kidete kulinda, kutetea na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu
kweli za Kiinjili, kwa kutambua kwamba, Familia ni Habari Njema ya watu wanaoishi
katika ulimwengu mamboleo na kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia: Kwa hakika,
watu wengi wanashindwa kuonja upendo, kiasi kwamba, wanajikuta wakielemewa na upweke
hasi.
Kanisa lina uzoefu na mang’amuzi makubwa katika hija ya maisha ya mwanadamu.
Linatambua ni kwa kiasi gani watu wanaendelea kuathirika kutokana na kumezwa mno na
malimwengu pamoja na kukumbatia utamaduni wa kifo; hali inayowafanya kutetea vitendo
vya utoaji mimba, kifo laini bila kusahau mateso na mahangaiko wanayopata wazee wasiokuwa
na msaada kutoka katika familia zao.
Kanisa linatambua kwamba, Familia inaundwa
kati ya Bwana na Bibi na Watoto ni matunda ya uhusiano wa dhati kati ya mume na mwanamke
na kwamba, watoto hawa wanahitaji kulindwa, kuheshimiwa na kuelimishwa. Ndiyo maana
Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utambulisho wa familia kadiri
ya mpango wa Mungu, dhidi ya tabi ana tamaduni zinazotaka kudhalilisha mwono huu kwa
kutaka kukumbatia ndoa za watu wa jinsia moja. Hili ni jambo ambalo kwa sasa linaendelea
kupigiwa debe katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.
Kanisa kwa
njia ya mikakati yake ya kichungaji, litaendelea kuenzi tunu bora za maisha ya kifamilia
pamoja na kuitetea taasisi hii katika majukwaa ya kimataifa; kwa kuangalia pia tamaduni,
ili tamaduni hizi ziweze kuenzi tunu bora na maisha ya kifamilia, ili ziweze kuleta
mvuto na mguso katika maisha ya watu wengi ndani ya Jamii. Familia inapaswa pia kuangaliwa
katika mtazamo mpana zaidi, kwa kukumbatia familia yote ya binadamu inayoundwa na
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.
Askofu mkuu Vincenzo
Paglia anasema kwamba, Baraza la Kipapa la Familia kwa sasa linajiandaa kwa ajiliya
Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa yatakayofanyika Jimbo kuu la Philadelphia,
Marekani, kunako Mwaka 2015. Katika kipindi hiki chote cha maandalizi, kutafanyika
tafakari ya kina kuhusu changamoto zilizotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji
Mpya iliyofanyika mjini Vatican, Mwezi Oktoba 2012 pamoja na Mafundisho ya Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita kwa viongozi waandamizi na hotuba yake kwa Mahakama kuu
ya Vatican.
Mwaka 2013 Jumuiya ya Kimataifa inajiandaa kuadhimisha Miaka 30
tangu Baraza la Kipapa la Familia lilipochapisha kwa mara ya kwanza Tamko la Haki
za Familia na Miaka 20 tangu Umoja wa Mataifa ulipoanzisha Siku ya Familia Kimataifa.
Tamko hili litawasilishwa kwenye Umoja wa Mataifa na kwenye Makao Makuu ya Mashirika
ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva bila kusahau Bunge la Ulaya.
Baraza la Kipapa
la Familia linaandaa Kongamano la Kimataifa la Wanasheria Wakatoliki litakalofanyika
mjini Vatican mwishoni mwa Mwezi Juni, 2013. Lengo ni kuwajengea uwezo wasomi na wanazuoni
kutafakari kwa kina kuhusu haki za familia katika mapambazuko ya Karne ya 21. Mkutano
mkuu wa Baraza utakaofanyika mwezi Oktoba 2013 utatafakari tena Tamko la Haki za Familia;
ili ziweze kufahamika na kusambazwa zaidi. Kuna maandalizi maalum ya semina zitakazokuwa
zinajadili umuhimu wa majadiliano ya kifamilia, kwa kuwashirikisha mabingwa kutoka
medani mbali mbali za maisha ya kijamii, ili kwa pamoja kuangalia kwa makini changamoto
zinazoibuliwa katika maisha ya ndoa na familia.
Familia ni taasisi ya kwanza;
changamoto katika elimu na makuzi; wazee na tasaufi ya wazee pamoja na dhana ya ushirikishwaji,
ni baadhi tu ya mada zinazoendelea kupikwa na Baraza la Kipapa la Familia, kama anavyobainisha
Askofu mkuu Vincenzo Paglia wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari hivi
karibuni.
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, familia kutoka sehemu mbali
mbali za dunia, zinatarajiwa kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro kuanzia tarehe
26 hadi 27 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, ili kwa pamoja kuweza
kumshukuru Mungu kwa zawadi, maisha na utume wa Familia kama chombo cha kufundisha
na kurithisha imani katika Jamii.