2013-03-13 07:21:00

Mabadiliko katika Liturujia za Kipapa


Monsinyo Guido Marini mshereheshaji wa Liturujia za Kipapa anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, tarehe 18 Februari 2013 aliruhusu kufanya marekebisho katika Ibada ya mwanzo wa utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo kuu la Roma anayepewa dhamana ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. RealAudioMP3
Papa mpya anawajibika kutembelea Makanisa makuu yaliyoko mjini Roma, yaani: Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu pamoja na Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma.
Kabla ya mageuzi yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Papa Mpya baada ya kuchaguliwa tu, siku ya pili alikuwa analazimika kwenda kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Kwa sasa Baba Mtakatifu anaweza kutembelea Kanisa hilo pale atakapoona inafaa kadiri ya taratibu zake. Tukio hili litafanyika nje ya Ibada ya Misa Takatifu.
Baba Mtakatifu Mpya atakapoanza utume wake rasmi, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu itakayohudhuriwa na Makardinali wote watakaokuwepo na baadaye watakula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Itakumbukwa kwamba, mara tu baada ya uchaguzi kwenye Kikanisa cha Sistina, Makardinali wanakula kiapo cha utii kwa Khalifa Mpya wa Mtakatifu Petro. Tendo hili linachukua mwono wa hadhara katika Ibada pamoja na kukazia ile dhana ya Kanisa moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume.
Haitakuwa kwa mara ya kwanza kwa Ibada hii kufanyika kwani Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili aliianzisha na imeendelea kuwa ni kumbu kumbu ya pekee katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mabadiliko mengine yaliyofanywa katika Ibada za Kipapa ni ile ya kuwatangaza wenyeheri kuwa watakatifu, Mkesha wa Pasaka pamoja na Ibada ya kuwavisha Palio takatifu Maaskofu wakuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.