Kikundi cha Waasi cha Seleka, Jamhuri ya Afrika ya Kati kinatishia maisha!
Askofu Juan Josè Aguirre Munos wa Jimbo la Bangassou, Jamhuri ya Afrika ya Kati anasema
kwamba, machafuko ya kivita yanayoendelea nchini mwake yanaendelea kusababisha madhara
makubwa kwa watu na mali zao.
Kikundi cha Waasi wameanza kufanya uvamizi na
kupora mali za watu na Kanisa na kuelekea mpakani na Sudan. Lengo la kikundi hiki
cha waasi ni kutaka kuipindua serikali na kuanzisha serikali itakayosimamiwa na sharia
za dini ya Kiislam.
Kujiimarisha kwa kikundi hiki kunaonekana kwamba, kinapata
msaada wa hali na mali kutoka nje ya nchi kwa malengo binafsi, kama inavyojionesha
nchini Mali. Ingawa kuna vikosi vya kulinda amani kutoka Mali na Afrika ya Kusini,
lakini Kikundi cha Waasi wa Seleka linadhibiti asilimia 80 hadi 90% ya nchi ya Afrika
ya Kati. Kikundi hiki kinaendelea kuleta uharibifu mkubwa katika miundo mbinu na nyaraka,
kiasi kwamba, historia ya wananchi wengi iko mashakani.