Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha Upendo, Umoja na Mshikamano wa Kanisa
Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumanne tarehe 12 Machi 2013 ameongoza
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili
ya kuombea uchaguzi wa Papa Mpya, kielelezo makini cha upendo, umoja na utume wa Khalifa
wa Mtakatifu Petro. Waamini wamekusanyika kwa ajili kumwabudu, kumshukuru na kumwomba
Mwenyezi Mungu, ambaye kwa njia ya upendo wake ameendelea kulisimamia, kuliongoza
na kuliimarisha Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Kardinali Sodano amemshukuru
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa uongozi wake makini kwa Kanisa na kwamba,
sasa Makardinali wanaanza uchaguzi wa Papa wa 265. Kanisa linamwomba Mwenyezi Mungu
aweze kulikirimia Kiongozi mwema kwa ajili ya Kanisa lake. Huyu ndiye anayetumwa kuwahubiria
wanyenyekevu Habari Njema ya Wokovu; kuwaganga wale waliovunjika moyo, kuwatangazia
mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari ya kufunguliwa kwao, kutangaza Mwaka
wa Bwana uliokubalika.
Kardinali Sodano anasema kwamba, utabiri huu umepata
utimilifu wake kwa njia ya Yesu Kristo, aliyekuja kuwaonjesha watu upendo wa Mungu,
kwa wote wanaoteseka, wanaokabiliana na ukosefu wa haki msingi za binadamu, umaskini
pamoja na kumong'onyoka kwa maadili na utu wema. Wote hawa wanahitaji kuona huruma
ya Mungu, utume ambao unatekelezwa na viongozi wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee
na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ambaye baada ya kuonesha upendo mkuu kwa Kristo, alikabidhiwa
dhamana ya kuwachunga Kondoo wake. Hii ni huduma ya upendo inayotekelezwa mintarafu
mwanga wa Injili na nguvu ya neema.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
katika Ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2013 alibainisha kwamba, kilele cha matendo
ya huruma kinajionesha kwa njia ya Uinjilishaji; yaani huduma ya Neno la Mungu pamoja
na adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, linalowahusisha na kuwachangamotisha Watu
wa Mungu kujenga na kuimarisha uhusiano na Muumba wao.
Uinjilishaji ni kielelezo
cha hali ya juu kabisa cha huduma kwa binadamu na kwamba, Yesu Kristo ni nguzo msingi
katika mchakato wa maendeleo endelevu, kama alivyobainisha Papa Paulo wa sita, katika
Waraka wake juu ya Maendeleo ya Watu.
Kardinali Angelo Sodano anasema kwamba,
Neno la Mungu limefafanua kwa dhati kabisa juu ya Fumbo Kristo na Kanisa lake; umuhimu
wa kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa, kila mtu kadiri ya karama aliyopokea, akitekeleza
wajibu wake katika fadhila ya upendo na amani. Umoja huu unasimikwa katika utofauti
wa karama na majukumu, lakini kwa pamoja unapania kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili
wa Kristo, yaani Kanisa.
Huu ndio umoja unaojengwa na kuimarishwa na Roho
Mtakatifu na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kielelezo wazi cha umoja wa Kanisa,
changamoto kwa kila mwamini kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa umoja wa Kanisa.
Kardinali
Sodano anasema amri kuu ambayo Kristo aliwaachia mitume wake, ile siku iliyotangulia
kuteswa kwake ni upendo. Huu ndio mhimiri mkuu wa Viongozi wa Kanisa, wanaosukumwa
kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ndugu zao katika Kristo. Huu ni wajibu mkubwa
kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro anayepaswa kuonesha upendo huu kwa Kanisa zima anapotekeleza
wajibu wake wa kuwaongoza Watu wa Mungu na Ulimwengu katika ujumla wake, daima akitafuta
kudumisha na kuimarisha misingi ya haki na amani.
Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita anasema, huduma ya upendo ni asili, utume na utambulisho wa Kanisa,
lakini kwa namna ya pekee, Kanisa la Roma, ambalo kimsingi ni kielelezo cha upendo.
Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali anahitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika
waamini kusali kwa ajili ya kuombea mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya, atakayetekeleza
utume huu nyeti katika Kanisa.