2013-03-11 09:43:41

Waamini wanaalikwa kuliishi tukio la Conclave kwa jicho la imani na matumaini


Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican katika tahariri yake kwa juma hili anasema kwamba, Makardinali katika mikutano yao kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wamepata fursa ya kubadilishana mawazo, mang'amuzi na vipaumbele vya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kwa hakika, wamefikia ukomavu na kwa sasa wako tayari kila mtu akiwajibika barabara kuanza hatua ya mwisho ya mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya, kwa kumwangalia Kardinali ambaye atakabidhiwa dhamana ya kuliongoza Kanisa la Kristo. Huyu ni kiongozi mwenye dhamana kubwa kwa ajili ya Kanisa la Kristo lililoenea sehemu mbali mbali za dunia; atakayekuwa na wajibu wa kuonesha dira na mwongozo wa maisha ya kiroho; kimaadili na kiutu. Ni kiongozi anayepaswa kuwasaidia wale wanaomtafuta Kristo ili waweze kuonja uwepo wake endelevu katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Padre Lombardi anabainisha kwamba, Conlcave ni tukio ambalo waamini wanaalikwa kuliishi kwa imani na matumaini; wakijiweka mikononi mwa Mungu ili kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, aweze kulikirimia Kanisa kiongozi mkuu. Funguo za Mtakatifu Petro za kufunga na kufungua mbingu ziwekwe mikononi mwa mtu anayestahili na dhamana kubwa katika ulimwengu mamboleo. Hivi ndivyo alivyosema wakati wa uchaguzi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Makardinali baada ya kujadili na kupembua maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, sasa wako tayari kujitosa kimaso maso kuingia katika Kikanisa cha Sistina kuanza uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kusali daima kwa ajili ya kuwaombea Makardinali ili waweze kutekeleza wajibu wao kikamilifu, ili hatimaye, Kanisa liweze kupata kiongozi ambaye atakuwa ni mchungaji, mtu mwema na mtakatifu, shahidi amini wa tunu msingi za Kiinjili.







All the contents on this site are copyrighted ©.