2013-03-11 08:29:31

Makardinali wako tayari kwa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro


Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumanne tarehe 12 Machi 2013, saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, itakayohudhuriwa na Makardinali pamoja na Familia ya Mungu kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mkutano wa Makardinali umeamua kwamba, Kikao cha uchaguzi wa Papa Mpya kitaanza rasmi Jumanne, tarehe 12 Machi 2013. Majira ya saa 10:30 Jioni kwa saa za Ulaya, Makardinali wataingia kwenye Kikanisa cha Paulo, tayari kuingia kwenye Kikanisa cha Sistina, wakiongozwa na nyimbo za kuomba mapaji ya Roho Roho Mtakatifu wanapoanza kutekeleza dhamana hii nyeti kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa la Kristo.

Kikao hiki kitaanza kwa Makardinali kula kiapo cha siri kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa. Conclave inapoanza, lango linafungwa na hapo waamini wanaendelea kuwasindikiza Makardinali kwa njia ya sala, wakisubiri kuona moshi mweupe alama kwamba, Kanisa limempata Papa Mpya!

Wakati huo huo, Maafisa na wote watakaohusika na shughuli za Conclave, tarehe 11 Machi 2013, majira ya jioni wanakula kiapo cha kutunza siri za uchaguzi wa Papa Mpya kama ilivyoamriwa na sheria pamoja na kanuni za Kanisa. Ibada ya kula kiapo itafanyika kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Paulo.

Hawa ni Katibu wa Makardinali, Washereheshaji wa Ibada za Kipapa, Mapadre walioteuliwa kwa kazi maalum, Watawa wanaohudumia Sakristia, Madaktari na wauguzi, wafanyakazi wanaolinda usalama, wahudumu na wataalam. Kundi hili litajulishwa umuhimu wa tukio hili kwa maisha na utume wa Kanisa. Wataandika na kutamka wazi kiapo hiki mbele ya Kardinali Camerlengo, Tarcisio Bertone pamoja na mawakili wawili ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka.

Padre Federico Lombardi akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa juma, amefafanua kwamba, Makardinali wataanza kuingia kwenye vyumba walivyopangiwa kwenye Hosteli ya Sanctae Marthae iliyoko ndani ya mji wa Vatican, tarehe 12 Machi 2013, kuanzia saa 1:00 na kuendelea, ili kuwapatia nafasi ya kujiandaa kwa ajili ya kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hapo saa 4:00 asubuhi.

Mkutano wa Makardinali unaendelea hata Jumatatu, ili kutoa nafasi kwa Makardinali ambao walikuwa bado hawajashirikisha mawazo yao kuzungumza kabla ya kuanza rasmi mchakato wa kumchagua Papa Mpya. Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV kitarusha picha maalum katika matukio haya maalum wakati wahudumu wa Conclave wa kula kiapo kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya.








All the contents on this site are copyrighted ©.