2013-03-11 11:03:34

Kanisa nchini Zambia limeanzisha Kampeni dhidi ya nyanyaso na madhulumu kwa wanawake!


Madhehebu ya Kikristo nchini Zambia yameanzisha kampeni dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na dhuluma dhidi ya wanawake, hali ambayo kadiri ya takwimu za kitaifa zinaonesha kwamba, imefikia asilimia 47%. Wanawake na wasichana katika umri wa miaka 15 wameonja kipigo cha nguvu, wamedhalilishwa kijinsia na wakati mwingine, matukio kama haya yamepelekea wanawake hawa kupoteza maisha yao.

Kanisa Anglikani nchini Zambia kwa kushirikiana na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo limeamua kulivalia njuga tatizo la dhuluma na nyanyaso dhidi ya wanawake kwa kuwajengea uwezo utakaowasaidia kusimama kidete kutetea haki zao msingi, kwa kuwa na nguvu za kiuchumi. Kanisa Anglikani linasema kwamba, wanawake wakiwezeshwa kiuchumi, wataweza kuwa na nguvu na ari ya kupigania haki zao msingi na kamwe hawatakubali kunyanyasika.

Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwajengea wanawake uwezo pamoja na kuwapatia ushauri kwa kushirikiana na mashirika ya kitaifa na kimataifa, ili kuhakikisha kwamba, lengo hili linafikiwa. Mkakati huu unapania pia kuwapatia wanawake habari zaidi, zitakazowafungua macho na masikio ili kuona yale yanayotendeka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa hakika, Kanisa limeamua kuwa ni sauti ya wanawake wanaoonewa na kudhulumiwa nchini Zambia.

Bi Grazia Mazala Phiri, Mkurugenzi mkuu kitaifa wa Programme za Wanawake nchini Zambia, anabainisha kwamba, wanapenda kuwajengea wanawake uwezo, ili kuimarisha mahusiano ya kijamii pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama, ili wanawake waweze kutekeleza majukumu yao kwa amani na utulivu bila ya kunyanyasika.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Albert Chama wa Kanisa Anglikani, Jimbo kuu la Afrika ya kati anabainisha kwamba, Kanisa linapenda kuwaunga mkono wanawake, ili kuboresha maisha yao kwa njia ya elimu makini, ambayo kimsingi ni mkombozi wa wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.