2013-03-11 08:58:47

Jumuiya ya nchi za Ulaya inahamasishwa kuibua mikakati ya kupambana na baa la umaskini wa hali na kipato!


Jumuiya ya Ulaya haina budi kuwa na mwelekeo wenye uwiano katika masuala ya utawala yanayofumbata mwelekeo wa kijamii. Hii inatokana na ukweli kwamba, sera na mikakati ya kiuchumi iliyobuniwa hivi karibuni na nchi nyingi za Ulaya kama sehemu ya marekebisho ya hali mbaya ya uchumi, zimepelekea kuporomoka kwa hali ya maisha kwa wananchi wanaoishi katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Mikakati hii inapaswa kujikita katika ile azma ya kupambana na baa la umaskini na ukosefu wa usawa, mambo ambayo yanaendelea kuibuka kwa kasi kubwa Barani Ulaya. Hili ni tamko la pamoja lililotolewa na Shirikisho la Makanisa Ulaya pamoja na Tume ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya. Mkutano huu ambao umefanyika hivi karibuni, ni sehemu ya utaratibu wa Viongozi wa Makanisa kukutana na Marais Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Wajumbe hao pamoja na mambo mengine wameonesha wasi wasi unaoendelea kujitokeza Barani Ulaya kwa wananchi wengi kujikuta wakiogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato. Wanatambua kwamba, kuna haja kwa Serikali za Ulaya kuibua mikakati itakayofanikisha upatikanaji wa fursa za ajira ili kupunguza umati mkubwa wa vijana ambao kwa sasa hauna kazi, jambo ambalo ni hatari kwa maisha na usalama wa raia.

Viongozi wa Makanisa wamejadili pia umuhimu kwa wafanyakazi kupata nafasi ya kupumzika ili kujichotea nguvu ya kuweza kusonga mbele katika shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma kwa Jamii, kwa kuweka uwiano mzuri kati ya: mtu, kazi na familia. Marekebisho ya sera za kiuchumi Barani Ulaya yawashirikishe pia wadau wengine ili marekebisho haya yaweze kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi badala ya kuonekana ni kwa ajili ya wajanja wachache wanaotaka kujinufaisha na hali ngumu ya wananchi wengi.

Viongozi wa Makanisa wamejadili pia kuhusu ruzuku na misaada ya maendeleo inayotolewa kwa ajili ya Nchi changa duniani. Viongozi hawa wanataka kufanyike upembuzi uakinifu ili kubaini nchi ambazo kwa sasa hazihitaji kupata msaada kutoka nchi za nje na badala yake, kusaidia mchakato wa ukusanyaji wa kodi na mapato kutoka katika Makampuni ya Kimataifa kwa ajili ya mafao ya wengi badala ya mwelekeo wa sasa ambao Makampuni ya Kimataifa yanaendelea kufaidika kutokana na misamaha ya kodi, rushwa na ufisadi, vikwazo vikubwa katika uimarishaji wa utawala bora unaozingatia mafao ya wengi.

Umoja wa Ulaya usaidie katika mikakati ya maboresho ya ukusanyaji wa mapato na mifumo ya Benki. Lengo ni kujenga na kuimarisha misingi ya utawala wa sheria, ukweli na uwazi kwa ajili ya mafao ya wengi.








All the contents on this site are copyrighted ©.