2013-03-11 08:42:30

"Extra Omnes" Hairuhusiwi!


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, mara baada ya Makardinali wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura kula kiapo cha kutunza siri za uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, lango la Kikanisa cha Sistina litafungwa kwa maneno ya Kilatini “Extra Omnes” “Hairuhusiwi”.

Hapo Kardinali Prospero Grech, O.S.A., atatoa tafakari ya kina na kuanza kupiga kura ya kwanza kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa. Baadaye, Makardinali kwa pamoja watasali Masifu ya Jioni na kurudi kwenye Hosteli ya Sanctae Marthae kwa chakula cha usiku, sala na mapumziko.

Wakati wa Conclave Makardinali baada ya kupata kifungua kinywa, wataelekea kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Paulo kwa ajili ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Saa 3:30 asubuhi wanaingia kwenye Kikanisa cha Sistina na kusali masifu baadaye kuendelea na zoezi la upigaji kura. Saa 6:30 mchana wanarudi Hosteli kwa chakula cha mchana na mapumziko mafupi. 10:00 jioni Makardinali wanarudi tena kwenye Kikanisa cha Sistina kuendelea na zoezi la kupiga kura. Saa 1:15 shughuli zote za kupiga kura zinakamilika na kurudi kwa ajili ya chakula cha usiku, sala na mapumziko.

Hii anasema Padre Federico Lombardi, ndiyo ratiba elekezi wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya. Wakati wote huo, bila shaka macho na masikio ya watu wengi yatakuwa yanaelkezwa mjini Vatican kufahamu kile kinachoendelea. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican imejipanga vyema kuhakikisha kwamba, inakupasha hatua kwa hatua mchakato mzima.

Makardinali 133, katika mkutano wao elekezi wamejadili pamoja na mambo mengine: matarajio ya wasifu wa Papa Mpya, shughuli na utume wa Mabaraza ya Kipapa pamoja na changamoto ya kufanya maboresho makubwa katika idara za Vatican, kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa la kiulimwengu. Makardinali wamehabarishana kuhusu hali ya maisha sehemu mbali mbali za dunia pamoja na changamoto wanazoendelea kukabiliana nazo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Padre Lombardi amewaambia waandishi wa habari kwamba, ile Pete ya Mvuvi na Mihuri yote iliyokuwa inatumiwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, imeharibiwa na haiwezi kutumika tena, bali itahifadhiwa. Pete yenye alama ya Mashua ya Mtakatifu Petro, Nyavu na Jina la Khalifa wa Mtakatifu Petro atakayechaguliwa itatengenezwa tena.

Kutakuwa na ulinzi maalum kwenye maeneo yote yanayohusika moja kwa moja na uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Jambo la msingi kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, ni kuendelea kusali kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.








All the contents on this site are copyrighted ©.