2013-03-09 10:10:11

Mkusanyiko wa Mahubiri ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI siku chache kabla ya kung'atuka kutoka madarakani zimechapishwa katika kitabu!


Idara ya uchapaji ya Vatican imechapisha kitabu ambacho kinajulikana kwa jina "I Have Never Felt Alone" "Sijawahi Kamwe Kujisikia Upweke", maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita wakati wa Katekesi aliyoitoa hapo tarehe 27 Februari 2013, Siku moja kabla ya kung'atuka kutoka madarakani.

Ni kitabu kinachoonesha maneno ambayo yatabakia kuwa ni wosia wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kabla ya kutoweka katika maisha ya hadhara, ili kupanda kwenda Mlimani kusali na kufanya tafakari ya kina. Hii siku ambayo umati mkubwa wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia ulimiminika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kuonesha upendo na mshikamano kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyeliongoza Kanisa kwa imani, busara na hekima kubwa katika kipindi chote cha miaka minane ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Nyuma ya Kitabu kumeandikwa maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, aliposema kwamba, sasa yeye ni hujaji wa kawaida anayeanza hatua ya mwisho ya maisha yake hapa duniani. Huu ni mchango wa Idara ya Uchapaji ya Vatican kwa kutambua na kuthamini utume wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ambaye ameridhia mwenyewe kutoa utangulizi wa kitabu hiki.

Idara ya Uchapaji ya Vatican imekuwa bega kwa bega na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, ameitumia idara hii kama chombo cha kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Kitabu kina hotuba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyoitoa kwa Makardinali hapo tarehe 11 Februari 2013 akionesha utashi na uhuru kamili wa kung'atuka kutoka madarakani ifikapo tarehe 28 Februari 2013. Kuna Katekesi ya kina, ambayo kimsingi ni muhtasari wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, aliyoitoa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano ya Majibu, jioni aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na kutoa mahubiri ambayo yanaendelea kutoa mwangwi katika maisha na utume wa Kanisa. Tarehe 28 Februari 2013, Baba Mtakatifu alizungumza na Makardinali, hotuba ambayo pia iko kwenye Kitabu hiki.

Idara ya uchapaji ya vatican inafafanua kwamba, kitabu hiki kina waraka wa kichungaji kuhusu mabadiliko ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa sasa kinatolewa katika lugha ya Kiitalia.







All the contents on this site are copyrighted ©.