Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alifanya marekebisho makubwa katika Sheria
na Katiba ya Kitume Pastor Bonus, iliyokuwa imetolewa na Papa Yohane Paulo wa Pili,
kunako mwaka 1988. Waraka huu mpya
unaojulikana kama Ministrorum Institutio uliotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa
kumi na sita unahamisha: dhamana na madaraka ya Seminari kutoka katika Baraza la Kipapa
la Elimu Katoliki na kuyapeleka katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri. Baba
Mtakatifu anasema, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walionesha umuhimu wa
Mama Kanisa kujikita katika majiundo makini ya Makleri mintarafu Sheria na Kanuni
za Kanisa, ili hatimaye, waweze kutekeleza wajibu wa kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha
watu wa Mungu. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Seminari likapewa dhamana ya kuhakikisha
kwamba, Waseminari wanapata majiundo makini kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto
wa Nane, katika Waraka wake wa Creditae Nobis wa Mwaka 1725. Kanisa likaendelea kutoa
kipaumbele kwa majiundo ya waseminari kwa kufanya marekebisho mbali mbali yanayojionesha
kwa namna ya pekee katika Sheria za Kanisa za Mwaka 1917. Katika Muswada wa Sheria
Mpya za Kanisa, matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, iliamriwa kwamba, maelezo
kuhusu majiundo ya Waseminari yawe ni sehemu ya utangulizi kuhusu sheria na kanuni
za Kanisa kuhusiana na wito wa Upadre. Hii ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa
hatua mbali mbali za malezya maisha na wito na Kipadre. Baba Mtakatifu Yohane Paulo
wa Pili katika Waraka wake wa kichungaji, Pastor Dabo Vobis wa Mwaka 1992 anakazia
umuhimu wa kutambua na kuheshimu uhusiano uliopo kati ya majiundo makini kabla ya
kupewa Daraja Takatifu, wakati wa kupewa sanjari na Majiundo endelevu ya Kipadre.
Lengo ni kuendeleza mshikamano wa upendo na utume miongoni mwa Mapadre wenye umri
tofauti. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, ni kutokana na
sababu hizi msingi kuhusu majiundo na malezi ya kipadre; maisha na utume wa Mapadre
na Mashemasi, ameamua kuhamishia dhamana na utume huu katika Baraza la Kipapa kwa
ajili ya Makleri. Baraza hili litakuwa na dhamana ya kuhamasisha, kutunza na kuchagua
wale wanaofaa kwa ajili ya maisha na wito wa Kipadre. Baraza ltajikita pia katika
maisha ya mtu mzima: kiutu, kiroho, kielimu na kuainisha mikakati ya shughuli za kichungaji
zinazotekelezwa katika Seminari na Nyumba za Malezi na Majiundo ya Kipadre. Litashughulikia
pia majiundo endelevu ya Mapadre na Mashemasi wa kudumu, ili kuwawezesha kutekeleza
kwa umakini mkubwa utume wao pamoja na kuzingatia masilahi yao ya kijamii.