Kanisa Katoliki Tanzania linaendelea kutimua vumbi katika sekta ya elimu ya juu!
Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano maalum
na Radio Vatican wakati huu Kanisa Katoliki nchini Tanzania linapoadhimisha Miaka
150 tangu Wamissionari wa kwanza walipotua Visiwani Zanzibar, huo ukawa ni mlango
wa Imani kwa Kanisa Katoliki, linajivunia mchango wake katika sekta ya elimu nchini
Tanzania.
Anasema, kwa
hakika Kanisa limekuwa ni mdau mkuu wa maendeleo ya elimu nchini Tanzania kuanzia
katika shule za awali, msingi, sekondari, vyuo na sasa linaendelea kucharuka katika
mchakato wa maboresho ya elimu ya juu. Hii ni changamoto iliyotolewa na Mapadre, Watawa
na Waamini waliokerwa na uduni wa elimu ya Tanzania kwa wakati huo, wakaamua kulivalia
njuga tatizo hili kwa kuwekeza katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania,
SAUT, leo hii, anasema Askofu mkuu Lebulu, kinatimua vumbi nchini Tanzania! Wengi
walidhani kwamba, hii ilikuwa ni nguvu ya soda, lakini matunda yake yanaendelea kujionesha
sehemu mbali mbali za Tanzania.
Alipohojiwa kuhusu "siri ya mafanikio haya"
Askofu Mkuu Lebulu hakusita kusema kwamba, ni jeuri, ari na hamasa iliyotolewa na
Mapadre pamoja na Watawa walioamua kwa dhati kabisa kuwekeza katika uongozi bora,
wakitafuta mafao ya watanzania wengi; wakaonesha mipango na mikakati endelevu kwa
ajili ya maboresho ya sekta ya elimu ya juu nchini Tanzania. Wakatafuta, wakakusanya
na kuzalisha fedha kwa ajili ya ustawi wa elimu Tanzania. Fedha hii imetumika barabara
na matokeo yake ni kuendelea kupanuka kwa SAUT sehemu mbali mbali za Tanzania!
Hawa
ni Mapadre waliotambua na kudhamiria kuendesha sekta ya elimu chini ya uongozi na
usimamizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kuongoza kisayansi na hivyo
kuingia katika ushindani wa soko la elimu ya juu kisayansi, wakiwa na lengo la kuwapatia
watanzania wenzao elimu iliyo bora zaidi, itakayowasaidia kupambana na mazingira yao,
ili Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!
Askofu mkuu Josephat Lebulu anakiri kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania
lilisinzia kidogo katika kuwekeza kwenye mfumo wa elimu ya juu, lakini baada ya kutambua
umuhimu wake, leo hii linaendelea kutimua vumbi! SAUT, haishikiki!