Kuanzia karne ya kumi na moja, historia ya Kanisa Katoliki inaonesha kwamba, kulikuwepo
na kiongozi aliyejulikana kama “Camera thesauraria” “Mhazini wa Kanisa” aliyepewa
dhamana ya kuratibu masuala ya fedha na mali ya Kanisa.
Dhamana hii kwa sasa
inatekelezwa wakati ambapo kiti cha ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi, kama ilivyo
kwa wakati huu, baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kung’atuka kutoka
madarakani hapo tarehe 28 Februari 2013.
Kunako Karne ya 12 mkuu wa Ofisi hii
alijukana kama “Camerarius” au Camerlengo. Kadiri ya miaka ilivyozidi kuyoyoma, Camerlengo
ambaye kwa Kiswahili chepesi tungeweza kusema, “Mlinzi” au “Mratibu” akapewa dhamana
kuwa Katibu mkuu wa shughuli za Kanisa pamoja na kushughulikia masuala ya sheria na
kesi mbali mbali. Ni kiongozi aliyekuwa juu ya Mahakama zote zilizokuwa chini ya Vatican.
Tarehe 29 Juni 1908 Papa Pio wa tisa, katika Waraka wake wa kichungaji “Sapienti
Consiglio” akamrudishia Caerlengo madaraka aliyokuwa nayo kwa miaka iliyopita, yaani
kusimamia fedha na mali ya Kanisa wakati ambapo kiti cha ukulu wa Mtakatifu Petro
kiko wazi.
Kunako mwaka 1967 Papa Paulo wa sita, katika Waraka wake wa kichungaji
“Regimi Ecclsiae Universe, alibainisha kwamba, ikiwa kama Camerlengo anazuiliwa kutekeleza
wajibu wake kisheria, basi msaidizi wake afanye kazi kuanzia pale ambapo kiti cha
ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi hadi uchaguzi wa Papa Mpya. Mwenyeheri Yohane Paulo
wa Pili katika Waraka wake wa kichungaji “Pastor Bonus wa mwaka 1988 akathibitisha
tena dhamana hii.
Kunako mwaka 1996, Papa Yohane Paulo wa Pili akatamka wazi
katika Waraka wake wa kichungaji “Universi Dominici Gregis” kwamba, ni viongozi wakuu
wawili tu ambao nyadhifa zao haziwezi kukoma wakati ambapo kiti cha ukulu wa Mtakatifu
Petro kiko wazi. Hawa ni Camerlengo na Mhudumu mkuu wa Toba.
Itakumbukwa kwamba,
kwa sasa Camerlengo ni Kardinali Tarcisio Bertone aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, tarehe 22 Juni 2006 kuwa Katibu mkuu wa Vatican. Tarehe 4 Aprili
2007 akamteuwa pia kuwa ni Camerlengo. Kwa mara ya kwanza, alianza kutekeleza wajibu
wake huu nyeti, tarehe Mosi, Machi 2013 baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita kung’atuka kutoka madarakani.
Mkaguzi mkuu msaidizi wa fedha na mali
ya Kanisa ni Askofu Giuseppe Sciacca, ambaye naye anajulikana kama Camerlengo msaidizi.
Viongozi hawa wawili wanasaidiwa na jopo la Dekania ya Mapadre wanane. Ni matumaini
ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwamba, walau kwa sasa umeweza kupata fununu
yak ile kinachoendelea ndani ya Kanisa wakati huu Kanisa linaposali kwa ajili ya kuwaombea
Makardinali ili waweze kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, atakayeliongoza Kanisa
katika kipindi hiki cha mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Makala
hii imeandaliwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.