2013-03-08 12:42:17

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yana laani dhuluma na nyanyaso dhidi ya wanawake, yanataka wawezeshwe zaidi katika sekta ya kilimo!


Tamko la pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa linabainisha kwamba, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kimataifa, kwa mwaka 2013 iwe ni fursa ya kulaani vitendo vyote vinavyosababisha dhuluma na nyanyaso kwa wanawake sehemu mbali mbali za dunia na hivyo kuanza mchakato wa kuwajengea uwezo katika sekta ya kilimo, ili waweze kuzalisha zaidi na hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.

Wakuu wa Mashirika haya wanasema kwamba, licha ya wanawake kuwa ni wadau wakuu wa uzalishaji wa mazao ya chakula, lakini bado Jumuiya ya Kimataifa haijatoa kipaumbele cha kutosha kinachoonesha uhusiano wa karibu kati ya jinsia, madhulumu na uhakika wa usalama wa chakula. Haya ni mambo ambayo yameendelea kusababisha ubaguzi kiasi kwamba, waathirika wakubwa ni wanawake na wasichana wanaoishi vijijini.

Baadhi ya wasichana wanalazimishwa kuolewa wakiwa bado na umri mdogo; wajane na wanawake wanaendelea kukabiliana na mfumo dume unaowanyima haki zao msingi, hali inayokwamisha uzalishaji wa chakula. Jumuiya ya Kimataifa inataka wanawake na wasichana wawe na mazingira bora zaidi yatakayowawezesha kupata fursa ya elimu, ili kufanya maboresho katika medani mbali mbali za maisha, ili hatimaye, kushiriki katika kujiletea maendeleo endelevu.

Wanawake wanaunda walau asilimia 40% ya nguvu kazi katika sekta ya kilimo katika nchi zinazoendelea duniani. Jitihada za kuwajengea uwezo katika kilimo kuna maanisha maboresho makubwa katika tija na uzalishaji, hali ambayo itachangia kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula. FAO inataka kuhakikisha kwamba, inapambana kung'oa mambo yanayopelekea uwepo wa baa la njaa duniani.

IFAD inabainisha kwamba, inataka kuwajengea uwezo wakulima wadogo wadogo vijijini kuzalisha na kujipatia kipato kikubwa zaidi ili kuboresha maisha yao kwa njia ya mikopo midogo midogo. IFAD imetenga kiasi cha dolla za kimarekani millioni 14.8 kwa ajili ya mikopo kwa wakulima wadogo wadogo. Lengo ni kuwawezesha wakulima zaidi ya millioni 400 kupambana na baa la umaskini wa kipato na hali.

WFP inataka kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata chakula cha kutosha kwani kila mwaka inatoa chakula cha msaada kwa watu millioni 90 katika nchi 70 duniani.

IDLO inaziwezesha serikali na wananchi kufanya mabadiliko katika sheria ili kuimarisha: haki, amani na kukuza jitihada za maendeleo endelevu kwa kufaidika na fursa mbali mbali za kiuchumi. Hili ni Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na utawala wa sheria.









All the contents on this site are copyrighted ©.