Waadhama Makardinali wanaendelea na Mkutano wao hapa Vatican , ambamo Ijumaa hii
majira ya asubuhi walifanya kikao cha saba. Mkurugenzi wa kitengo cha habari
Vatican, Padre Federico Lombardi, kama kawaida yake, majira ya mchana alitoa muhtasari
kwa wanahabari, juu ya yaliyofanyika katika kikao hiki cha saba cha Makardinali.
Katika maelezo yake, alionyesha uwezekano wa Makardinali kuchagua tarehe ya kuanza
vikao vya kumchagua Papa, kinachoitwa Conclave. Na kwamba kuna mwelekeo mkubwa wa
Conclave kuanza mapema wiki ijayo. Asubuhi hii, jumla ya Makardinali 153 walishiriki
kikao , kati yao wapiga kura wakiwa 115. Padre Lombardi alitaja baadhi ya hoja
zilizojadiliwa , kwamba, ni pamoja na Katiba "Universi Dominici Gregis", ambamo
walitaka kujua, sababu msingi zilizo zuia makardinali walioshindwa kuhudhuria mkutano
huu. Aliwataja walioshindwa kufika ni Makardinali wawili, Kardinali Mstaafu Julius
Riyadi Darmaatmadja wa Jarkata, na Kardinali O'Brien, ambao wameomba udhuru kwa kutaja
sababu zilizowazuia ni pamoja na udhaifu wa mwili na pili ni sababu binafsi. Mkutano
wa Makadinali ulipiga kura na kukubali sababu zilizotolewa.
Aidha asubuhi
kulikuwa na vipengere 18 vilivyowasilishwa na kujadiliwa , kati yake ikiwemo mazungumzo
kati ya dini, maadiliviumbe, haki katika dunia. Pia walijadili furaha ya kutangaza
Injili na Huruma ya Mungu wakimrejea Mwenye Heri Papa Yohane Paulo II. Na pia walijadili
hoja ya ushirikiano na umoja katika decania ya Makardinali.