Domus Santae Mariae mahali watakapoishi Makardinali wakati wa uchaguzi wa Papa Mpya!
Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kunako mwaka 1996 aliamua kufanya ukarabati mkubwa
kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha ambayo kwa sasa inajulikana kama "Domus Santae
Marthae" iliyoko ndani kabisa ya Mji wa Vatican. Hili ni jengo lenye ghorofa tano
na lina vyumba 106 kwa ajili ya wageni maalum pamoja na vyumba 22 kwa matumizi ya
mtu binafsi.
Uongozi wa Hosteli hii unateuliwa na Katibu mkuu wa Vatican kwa
kuzingatia sheria na kanuni za Vatican. Kwa maneno mengine, huu ni Mfuko wa Mtakatifu
Martha kama ulivyonuiwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili.
Hapa ni mahali
panapotoa hifadhi na makazi kwa Makardinali, baadhi ya viongozi wanaofika mjini Vatican
kwa shughuli za kiofisi. Katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi wa Papa Mpya, wale
wote waliokuwa wanaishi kwenye Hosteli hii wameondolewa ili kutoa nafasi kwa Makardinali
watakaoshiriki katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baadhi ya viongozi watakaoruhusiwa
kuishi katika Hosteli hii ni wale waliotajwa kwenye Waraka wa Kichungaji kuhusu uchaguzi
wa Papa, unaojulikana kwa lugha ya Kilatini kama " Universi Dominici Gregis".
Jengo
hili lilijengwa na Papa Leo wa XIII kunako mwaka 1891, mwaka ambao unakumbukwa kutoka
na kuzuka kwa ugonjwa wa kipindu pindu kuzunguka viunga vya Mji wa Vatican na hivyo
kupelekea watu wengi kupoteza maisha yao. Wakati wa Vita kuu ya Pili wa Dunia, Jengo
hili lilitumika kwa ajili ya kutoa hifadhi kwa wakimbizi, Wayahudi na Mabalozi wa
Vatican kutoka katika nchi ambazo zilikuwa zimevunja uhusiano wa kidiplomasia na Italia.
Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alipokuwa anafungua Mfuko huu alibainisha
wazi kwamba, lengo ni kutoa huduma ya ukarimu kwa wageni wanaotembelea mjini Vatican,
ili waweze kuonja ule upendo na mshikamano wa kidugu unaopaswa kujionesha miongoni
mwa Makleri wanaotoa huduma yao kwenye Sekretarieti ya Vatican, wafanyakazi katika
Mabaraza ya Kipapa, Makardinali na Maaskofu wanaofanya hija zao za kitume ili kukutana
na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baadaye, iliamriwa kwamba, Jengo
hili wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, litatumiwa na Makardinali
wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura na wale wote waliotajwa katika sheria kwenye
mchakato huu. Viongozi hawa ni Katibu mkuu wa Makardinali, Mshehereshaji mkuu wa Liturujia
za Kipapa, Mapadre walioteuliwa kwa ajili ya kutoa Sakramenti ya Upatanisho katika
lugha mbali mbali.
Madaktari wawili kwa ajili ya kushugulikia dharura inapotokea.
Wapishi na wafanyakazi wa ndani. Wote hawa hawana budi kuthibitishwa na Kardinali
Camerlengo ambaye ndiye mratibu mkuu wa shughuli za Kanisa wakati ambapo kiti cha
ukulu wa Mtakatifu Petro, kiko wazi. Wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya,
Makardinali wanaweza kutembea kwa miguu kutoka katika Jengo hili kuelekea kwenye Kikanisa
cha Sistina, lakini pia kuna Bus maalum kwa ajili yao!