2013-03-07 07:16:50

Ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Mwaka 2013


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasema Kwaresima ni safari inayowajenga waamini katika Imani. Maaskofu wanachambua kwa kina na mapana hali halisi ya imani. Katika ujumbe wao, Maaskofu wanatoa pia fundisho la jumla: kwa kufafanua kuhusu imani, familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linayaangalia matukio makuu na muhimu katika maisha na utume wao wa Kanisa. Imani katika maisha ya kisiasa inapania kutafuta mafao ya wengi. Basi kwa muhtasari huu, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakutakia tafakari njema, ukiweza washirikishe pia jirani zako!

UTANGULIZI

Wapendwa Taifa la Mungu,

Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo… Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo… (Efe 1:2, 18-19).

“Simameni imara katika imani” tuliyoipokea kutoka kwa Mungu anayependa kutushirikisha maisha yake ya upendo. Imani ni njia pekee inayotuongoza katika upendo na muungano na Mungu. Ndiyo maana, sisi wachungaji wenu tunawaleteeni ujumbe huu wa Kwaresima kama sehemu ya wajibu wetu wa msingi, ili “kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo” (Kol 1:28). Katika maadhimisho ya Kwaresima ya mwaka huu, tunaungana na Mtume Paulo kuwahimizeni kwa msisitizo mkubwa na wa upendo tukisema tena: “Simameni imara katika imani” (1Kor 16:13). Hii ndiyo dira na mwaliko wa Kanisa kwa nyakati zote, na zaidi sana katika wakati wetu huu wa kihistoria ambapo kumejitokeza sana kuyumba kwa imani miongoni mwa waamini na hivi kuamsha uhitaji wa Uinjilishaji Mpya na wa kina kwa matendo. Tunapenda kuwashirikisha tafakari hii ili ituongoze sisi sote katika kuishi kiaminifu imani ile tunayoishiriki pamoja, imani ambayo baada ya kuipokea tunapaswa kuilinda, kuitunza na kuikuza. Tunataka mtambue siku zote kuwa sisi, kwa wajibu tuliopewa na Kanisa, tunapaswa kufundisha, kuilinda na kuifanya imani yenu ikue, na wala “si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu mnasimama” (2Kor 1:24).
Ni sala yetu kuwa, katika Mwaka huu wa Imani, tutafanya bidii ya makusudi kuijua, kuiishi na kuwashirikisha wengine imani yetu, ili “sote tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe” (Efe 4:13).
SURA YA KWANZA

KWARESIMA: SAFARI INAYOTUJENGA KATIKA IMANI
    “Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Habari Njema” (Mk 1:15). Haya ndiyo maneno ya kwanza ya Yesu, ambayo kadiri ya Mwinjili Marko, yanafungua utume wake Yesu. Hii ndiyo habari njema ya Kristo. Huo ndio msingi wa utume na muhtasari wa utume wa Mkombozi: kuujenga Ufalme wa Mungu ndani ya mioyo ya watu na miongoni mwa watu kupitia tendo la toba na imani.
  1. Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko wa kusafiri kiroho na Kristo Mwokozi wetu, kupitia njia ya toba na imani, ambayo kwayo mwanadamu anashiriki kuujenga Ufalme wa Mungu; ufalme wa upendo, wa haki na wa amani. Huu ni ufalme ambao “hata hivyo lengo lake la moja kwa moja ni usafi wa moyo, ambao bila huo hatuwezi kulifikia. Kwa hiyo tunapaswa kuwa na lengo hili akilini, na ikitokea kwamba kwa kipindi kifupi moyo wetu unaiacha njia hii ya moja kwa moja, tunapaswa kuirudia mara moja, tukiyaongoza maisha yetu kwa kulirejea lengo letu.”



    Kila Mwaka, Kanisa linaadhimisha fumbo la ukombozi wetu si kama kumbukumbu tu ya yaliyopita, bali uhalisia tunaopaswa kuuishi kila siku katika maisha yetu, na hivi kuendeleza tendo la ukombozi katika wakati wa sasa wa historia. Katika safari ya Kwaresima, Kanisa linatuongoza kwa tafakari na mazoezi yatakayotusaidia kukutana na Bwana Mfufuka aliye jiwe kuu la msingi la Ufalme wa Mungu. Kristo ndiye msingi wa imani yetu, imani ambayo “ni mwaliko wa uongofu wa dhati na ulio mpya kwa Bwana, na mwokozi pekee wa ulimwengu.” Huu ni mwaliko wa kuishiriki huruma kuu na upendo mkuu wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Huruma hiyo na upendo huo ndio unaotuwezesha kuyavuka maisha ya utu wa kale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele yetu (Rej. Fil 3:13).
  1. Safari ya maisha yetu, iliyo pia safari ya imani yetu, ni ndefu. Katika Agano la Kale, ililichukua Taifa la Israeli miaka arobaini kuingia katika Nchi ya Ahadi. Kipindi kirefu ambacho, pamoja na kutawaliwa na matendo makuu ya Mungu, kilitawaliwa pia na vishawishi vingi hata kuwafanya Waisraeli wafikirie mara kadhaa kuiacha safari iliyowaelekeza mbele kwenye Nchi ya Ahadi na kutamani kurudi nyuma, utumwani Misri. Kilikuwa kipindi kirefu kilichojaa hisia mchanganyiko wa furaha na shukrani (Rej. Kut 15:1-21); kipindi pia cha kutetereka kiimani na kukata tamaa kwa upande wa Waisraeli; hasa pale walipopata shida (Kut 14:10-12; Hes 11:4-6). Lakini pia kilikuwa ni kipindi kirefu kilichodhihirisha huruma na ustahimilivu wa Mungu; Mungu anayedumu kuwa mwaminifu kwa agano aliloweka na watu wake.

  2. Katika Agano Jipya, ilimchukua Yesu siku arobaini za kufunga ambamo ndani yake Yesu anayeshiriki hali yetu dhaifu, anatufundisha na kutuonesha njia ya kuvishinda vishawishi na dhambi. Safari hii ya Yesu ya siku arobaini ilikuwa ni kielelezo cha kipindi cha maisha yetu; maisha yanayoonja raha na karaha, yakidai kupokea yote hayo kwa jicho na uradhi wa moyo unaoongozwa na imani. Ni kwa jicho tu la imani ndipo tunaweza kung’amua uzuri wa mpango wa Mungu hata katika hali zile zisizofurahisha na kupendeza, kwani kwa njia hiyo tunaweza kukaa chini na kutafakari tukitafuta kujua ni ujumbe gani Mungu anataka kutufikishia kupitia matatizo na mateso yetu. Malezi haya ya kimungu mintarafu imani ni kile tunachojifunza juu ya ukuu na adhama ya imani kama njia ya kwanza na ya msingi kwa wokovu. Kujaribiwa kwake hakuna lengo jingine zaidi ya kuiimarisha na kuithibitisha. Mtume Yakobo anatukumbusha kuwa, “kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi” (Yak 1:3; Rej. 1Pet 1:7). Hivyo basi, ni matumaini yetu kuwa, pamoja na vikwazo na changamoto nyingi tunazopitia katika safari ya imani yetu, kipindi cha Kwaresima kinatupatia fursa ya mazoezi ya kiroho na tafakari zitakazotusaidia kukutana na Kristo Mfufuka.


SURA YA PILI

HALI HALISI YA IMANI
    Hali halisi ya kiimani katika wakati wetu huu inadhihirisha ubaridi wa imani (indifference), kutokupendelea mambo ya dini (agnosticism), mtazamo kwamba maoni binafsi ndiyo msingi na kipimo cha maadili na maamuzi ya maisha binafsi (relativism), na pia kutukuza malimwengu (secularism). Kipo pia kishawishi kikubwa cha kutaka kuugeuza ujumbe wa Injili kuonekana kuwa unafaa tu kuwabidisha wakristo kujihusisha na harakati za kijamii, kisiasa na kiutamaduni tu, bila yote haya kujengwa, kwa nafasi ya kwanza, juu ya imani kwa Kristo, aliye, kwanza kabisa, Bwana na Mwokozi wa Roho zetu. Kadiri siku zinavyokwenda, angalizo la Mwenyeheri Papa Yohane Paulo II linazidi kujidhihirisha wazi, kwani, “Vikundi vya wabatizwa vimepoteza hamu na ladha ya imani… havijitambui tena kuwa wanakanisa, vikiishi mbali na Kristo na mbali na Injili. Katika hali hiyo litatakiwa ‘tangazo jipya la Injili’ au ‘marudio ya Injili’.”
  1. Hali hii sio tu kwamba imezikumba nchi zile zilizobahatika kuuishi ukristo kwa karne nyingi, bali hata katika bara la Afrika, pamoja na kuonyesha dalili nyingi za kukua, bado imani imeonesha dalili nyingi za kutetereka. Lipo tatizo kubwa la ushirikina hata miongoni mwa wale wanaomwamini Kristo. Zipo sababu nyingi zinazochochea ushirikina. Moja ya sababu hizo ni umasikini wa waamini unaowapelekea kukosa elimu, afya na maisha bora. Mazingira kama haya yanafanya ushirikina ushamiri na kwa jinsi mtu anavyokuwa dhaifu katika imani, vivyo hivyo anaathirika vibaya na upepo wowote utakaovuma. Kizazi cha mtu aliye katika hali hii kinapokonywa fursa ya kurithishwa imani iliyo bora zaidi, kwani mazingira yanayotawala yanakuwa ni ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo kupitia nguvu za giza, ambazo ndiyo huduma waliyonayo karibu, kuliko kupitia nguvu za mwanga, kama elimu bora, afya bora na huduma za kiroho zilizo bora na karibu. Kundi la wale wanaojitangaza kutomwamini Mungu, hasa kati ya wasomi walioathiriwa na ushawishi wa kimagharibi, linazidi kukua pia. Zaidi sana ni kule kukosekana kwa malezi ya kina, huu ukiwa ni udhaifu, kwa upande mmoja wa wachungaji wasiotenga muda wao wa kutosha kwa ajili ya kutoa katekesi ya kina na endelevu kwa waamini, na kwa upande mwingine, ugumu wa waamini kutoa muda wao kufuata mafundisho ambayo yangewajenga kiimani. Athari ya malezi ya juu juu ya kiimani au ya watu kutopenda kufuata katekesi na mafunzo mengine ni kubwa sana. “Leo katika Afrika ‘malezi ya kiimani… mara nyingi hukomea katika kiwango cha chini sana, na dini nyingine kwa urahisi hunufaika katika ulegevu huu’.”

  2. Siku hizi inakuwa vigumu sana kumtofautisha mkristo na mtu mwingine yeyote asiye mkristo. Imekuwa dhahiri kwamba wote wanatenda uovu uleule na kufuata mienendo ile ile mibaya inayoshusha utu na hadhi ya mwanadamu. Udhaifu huu wa kushindwa kuiishi imani yetu kikamilifu unawafanya wakristo washindwe kumpa Mungu utukufu na sifa kwa njia ya matendo yao. Mt. Ireneo anasema: “Utukufu wa Mungu ni mwanadamu aliye hai kabisa.” Kwa maneno mengine, ndiyo kusema, utukufu wa Mungu ni mwanadamu kuishi kikamilifu, kwa utauwa, akiyachukulia maisha yake kuwa ni ushuhuda wa upendo wa Mungu duniani. Ukamilifu huu kwa mkristo unajidhihirisha katika tendo la kuiweka imani katika matendo ya kila siku. Ukamilifu huu unawezekana kwa sababu mkristo anamwamini Kristo aliyekuja ili ampatie uzima na awe nao tele; yaani, awe nao katika ukamilifu wote (Rej. Yn 10:10). Na Kristo huyu ndiye ambaye “ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu” (Yn 1:4). Kwa hivi safari ya imani ndiyo inayotuvusha kutoka katika hali ya ilimradi naishi tu na kuanza kuishi kikamilifu.

  3. Mwaka wa Imani kama ilivyokuwa kwa Sinodi ya 13 ya Kawaida ya Maaskofu iliyofanyika mwaka uliopita (2012), ni mwaliko kwa wakristo kurudia kuchukua uamuzi madhubuti wa kuiishi imani yao kikamilifu. Wakristo wanapaswa kutambua kuwa: “Bwana ndiye lengo la historia ya kibinadamu, ‘kitovu cha matarajio ya historia na ya ustaarabu’, kiini cha uzao wa kibinadamu, furaha ya kila moyo, na utimilifu wa matumaini yote.” Hili litadhihirika kama Wakristo tutaupokea kwa moyo radhi wito wa Mtume Yakobo anayesema: “Iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu” (Yak 1:22). Kwa sababu, “popote pale Mungu anapofungua mlango kwa neno ili kutangaza fumbo la Kristo (Rej. Kol 4:3), papo hapo anapaswa kuhubiriwa kwa ujasiri (Rej. 1Kor 9:16; Rum 10:14) na ushujaa mbele ya watu wote (Rej. Mdo 4:13. 29. 31…), Mungu aliye hai na Yule aliyemtuma kwa ajili ya wokovu wa wote, yaani Yesu Kristo.”


SURA YA TATU

FUNDISHO LA JUMLA


    “Simameni imara katika imani” (1Kor 16:13). Hivi ndivyo Mtume Paulo anavyowaandikia waamini wa Korintho. Anawahimiza wasimame imara katika imani ili wasije wakapoteza zawadi hiyo kubwa iliyo mlango wa zawadi zote za kimungu. Kanisa la Korintho lilikuwa limeanzishwa na Mtume Paulo mnamo mwaka 51. Baada ya kupanda mbegu ya imani katika mji wa Korintho, Paulo alikaa hapo mwaka mmoja na miezi sita (Mdo 18:11) akilijenga kanisa hili kwa mafundisho yake. Korintho ya wakati huo ilikuwa tayari ni mji mkubwa, wenye watu wengi na mchanganyiko, watu waliokuwa na uwezo na hadhi tofauti. Miaka mitano baada ya kuanzishwa kwa kanisa la Korintho, unajitokeza mpasuko mkubwa unaotishia kutokomeza imani changa ya waamini wa Korintho. Tatizo la kwanza lilikuwa ni mgawanyiko baina ya waamini walioanza kujiainisha kuwa ni wafuasi wa mtume huyu au yule (Rej. 1Kor 1:12-15). Ulianza pia kujitokeza ulegevu katika kufuata kanuni za ibada (1Kor 11:17-18); na utepetevu wa kimaadili (1Kor 1:12-15; 5:1-5; 6:12-20). Msingi wa imani ulipotikiswa, wakristo wa Korintho walifikia hatua ya baadhi yao kuanza kupinga ufufuko (1Kor 15:12). Katika hali hii ya upotofu ulioanza taratibu kuota mizizi. Mtume Paulo anasimama kidete kuwakumbusha kuwa “kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure” (1Kor 15:14). Mtume Paulo analihimiza Kanisa lirudi katika njia ya misingi ya imani aliyokuwa amewafundisha. Anawaambia Wakristo wa Korintho wakeshe na kusimama imara katika imani (Rej. 1Kor 16:13).
  1. Matatizo na migogoro iliyokuwa inalikabili Kanisa la Korinto ilitishia kuua imani changa ya waamini wa Korintho. “Kwa vipimo vya kibinadamu hali ya Korintho haikuwa na rutuba nzuri kwa upandaji wa imani na maadili ya kikristo, lakini kisichowezekana kwa akili ya binadamu, kiliwezekana kwa nguvu ya Mungu.” Paulo anayatafutia ufumbuzi matatizo ya jumuiya hii akijengea yote juu ya msingi wa imani.


Imani maana yake ni nini?
    Imani ni zawadi tunayopata kutoka kwa Mungu. Zawadi hii inakuwa ndilo jina la uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu katika mpango wa ukombozi. Kwake yeye aliyepokea zawadi na jina hili, imani inabeba maana yake halisi; yaani, imani, “ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr 11:1). Hii ni hali ya mwanadamu kuinua moyo na akili yake kumwelekea Mungu na ahadi zake, kwa maana sisi tunaomwamini Mungu “twaenenda kwa imani, si kwa kuona” (2Kor 5:7).
  1. Haya mambo “yatarajiwayo” na “yasiyoonekana” si nadharia isiyokuwa na msingi. Haya mambo “yatarajiwayo” na “yasiyoonekana” ni tamanio la kuishi katika muungano na Mungu, Mungu ambaye tumekwishamuona katika nafsi yake ya pili; yaani, katika Yesu Kristo. Kama Yesu mwenyewe anavyosema, “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yn 14:9), kwa sababu imani “ni jibu la mtu kwa Mungu ambaye anajifunua mwenyewe na kujitoa mwenyewe kwa mwanadamu.” Uhusiano huu mpya kati ya Mungu na mwanadamu ambao kwa njia ya Ubatizo, mwanadamu anafanyika kuwa mwana wa Mungu, unatuwezesha kutembea katika imani ya yale tunayoyatarajia katika ulimwengu ujao.

  2. Neno la Mungu na Sakramenti zake zinatufunulia njia za imani na zinakuwa ni hakikisho la kile tunachokiamini. Na kama anavyosema Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, “Kwa kusadiki na kujikabidhi kwa Mungu, tunaitikia neno la Mungu.” Mt. Ambrose anapowafundisha Wakristo wapya waliobatizwa mabadiliko yanayoendana na Sakramenti ya ubatizo waliyoipokea anasema: “Hapo awali mliona kwa macho ya mwili, sasa mnaona kwa macho ya moyo.” Hivi ndivyo wale wote waliompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wao wanavyotakiwa kuishi na kutembea kuelekea Ufalme wa Mungu. Kuona huku kwa macho ya moyo ndiyo kuona kwa imani. Hii ndio kusema anayeamini ameamua kujikabidhi kwa Mungu na anaahidi kuishi kiaminifu kadiri ya matakwa ya Neno la Mungu na ahadi zake. Tendo hili la imani kuu ya kusadiki pasipo kuona (Rej. Yn 20:29) lina tuzo lake, kama anavyotusaidia kung’amua Mt. Agostino anaposema: “Imani ni kuamini kile usichokiona, na tuzo ya imani hii ni kuona kile ulichoamini.”

  3. Imani ndio inayotupatia hakikisho la msingi ambalo juu yake tunayasimika maisha yetu yote. Imani inakuwa ni mlango usioweza kufungwa na yeyote. Kama tunavyosoma katika waraka wa sita kati ya nyaraka saba zilizoelekezwa kwa makanisa, kanisa la Filadelfia wanaambiwa: “Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga” (Ufu 3:8). Mlango huu daima uko wazi na kwa neema ya Mungu kila mtu anaweza kuupitia, iwapo tutakuwa tayari “kurekebisha maisha yetu kuendana na ukweli wa ulimwengu mpya.”

  4. Kanisa katika Mwaka huu wa imani linatuelekeza pia kukua katika imani kwa njia ya tafakari na kujifunza kwa kina Kanuni ya Imani; yaani, imani tunayoikiri. Kwa njia ya Sakramenti; yaani, imani tunayoiadhimisha. Kwa njia ya Amri Kumi za Mungu; yaani, imani tunayoiishi. Na kwa njia ya tafakari ya Sala ya Bwana; yaani, imani tunayoisali. Hivi ndivyo mafundisho ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki yalivyopangwa na kubainisha kwa ufasaha mkubwa muhtasari wa namna mkristo anavyotakiwa kuishi.


Imani kwa Mungu na kwa Neno lake
    “Nasadiki kwa Mungu mmoja”. Msingi wa imani yetu ni Mungu katika Nafsi Tatu; yaani, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mungu anayetupatia zawadi ya imani anatutaka tumtolee shukrani kwa kuiishi zawadi hii tukiwa tumeunganika naye katika Utatu wake Mtakatifu. Katika Injili ya Yohane, Yesu alipowaasa wafuasi wake wasikitendee kazi chakula kiharibikacho (Rej. Yn 6: 27) wao waliuliza wakitaka kujua wafanye nini basi: “Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?” (Yn 6:28). Hili ni swali ambalo tunaweza kulifanya kuwa letu katika kipindi hiki cha Mwaka wa Imani, na bila shaka, katika maisha yetu yote. Yesu anawajibu akisema: “Hii ndiyo kazi ya Mungu: mmwamini yeye aliyetumwa na yeye” (Yn 6:29). Humo ndimo ulimo utimilifu wote wa mpango wa Mungu anayejidhihirisha katika Utatu Mtakatifu. “Kukiri imani katika Utatu Mtakatifu – Baba, Mwana na Roho Mtakatifu – ni kuamini katika Mungu mmoja ambaye ni Upendo (rej. 1 Yn 4:8): Baba, ambaye katika utimilifu wa wakati alimtuma Mwanae kwa ajili ya wokovu wetu; Yesu Kristo, ambaye kwa fumbo la kifo chake na ufufuko aliukomboa ulimwengu; Roho Mtakatifu, ambaye analiongoza Kanisa katika karne zote tunaposubiri ujio mtukufu wa Bwana.”


    Imani kwa Mungu inakuwa ni tendo linalotuinua kupitia tendo la “utii wa imani”: “Utii wa imani lazima apewe Mungu anayejifunua (Rum 16:26; taz. Rum 1:5; 2Kor 10:5-6). Kwa imani mwanadamu hujikabidhi kikamilifu na kwa uhuru mikononi mwa Mungu, akitoa kwa Mungu mwenye kufunua “heshima kuu ya akili na utashi”, na akikubali kwa hiari ufunuo anaopewa na Yeye. Ili imani hii iweze kutekelezwa, mtu hana budi kutanguliwa na kusaidiwa na neema ya Mungu. Kadhalika hana budi kuwa na msaada wa ndani wa Roho Mtakatifu anayesukuma moyo na kumwelekeza kwa Mungu, na anayefunua macho ya akili na anayewapa “watu wote utamu katika kuukubali na kuuamini ukweli”. Roho Mtakatifu huyohuyo hukamilisha imani daima, kwa njia ya mapaji yake ili ufunuo ueleweke kwa undani zaidi.”


    Neno la Mungu linabaki kuwa ni msaada usiopimika unaotusaidia kung’amua kujifunua huku kwa Mungu. Imani yetu katika Kristo hulishwa kwa neno la Kristo mwenyewe. “Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Rum 10:17). Neno la Mungu linailisha imani yetu na kutupatia hakikisho la kile tusichokiona na kukigusa sasa kupitia milango yetu mitano ya fahamu. Imani inakuwa ni mlango wa sita wa fahamu ulio na umuhimu wa juu kwani inatusaidia kutamani yale ambayo jicho halijapata kuona wala sikio kusikia (Rej. 1Kor 2:9). “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu” (Rum 10:10).

Imani kwa Kanisa
    “Nasadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume”. Kanisa linabaki kuwa “Mama na Mwalimu” wa imani na ni chombo cha kimungu kinachowaunganisha watu na Mungu na baina yao. Kwa sababu hiyo Mt. Ireneo wa Lione anatukumbusha kuwa, “Lilipo Kanisa, yupo Roho wa Mungu: alipo Roho wa Mungu lipo Kanisa na neema zote.” Kwa maneno mengine ndio kusema, lilipo Kanisa la kweli lililoanzishwa na Kristo juu ya msingi wa Mitume hapo imani ya kweli ipo, kwa sababu, “Kanisa la Mungu aliye hai”, ni “nguzo na msingi wa kweli” (1Tim 3:15). Hata hivyo, ilipo imani hazikosekani changamoto. Kwa sababu, “hatusadiki tu kwa Kanisa, bali wakati huo huo sisi nasi ni Kanisa.” Tunatambua wazi kwamba huku kuwa Kanisa ni safari ya wongofu. Ni safari ya wongofu kwa kuwa ndani ya Kanisa wadhambi na watakatifu wanapata nafasi, lakini wote wakialikwa kukua katika njia ya wongofu. “Kanisa … ambalo huwakumbatia wakosefu ndani yake, na wakati uleule ni takatifu na linahitaji kutakaswa, haliachi kamwe kutubu na kujitengeneza upya.”
  1. Safari yetu ya kukua katika imani ndani ya Kanisa inaifanya nafasi ya Kanisa kwa wokovu kuwa ni ya muhimu sana. Umuhimu wake unatokana na ukweli kwamba lenyewe ni Mwili wa Fumbo (Kol 1:18) wa Kichwa ambaye ni Kristo mwenyewe. Ndiyo maana, Kanisa “ni mwezi wa kweli. Kutoka katika mwanga usiokuchwa wa nyota ya kidugu, linapata mwanga wa umilele na wa neema. Kimsingi, Kanisa haliangazi mwanga ulio wake kwa asili, bali mwanga wa Kristo. Kanisa linapata mng’ao wake kutoka kwenye jua la haki, ili baadaye liweze kusema: mimi ninaishi, lakini si mimi bali Kristo anaishi ndani yangu (Gal 2:).” Ni kutokana na uhusiano huu uliopo kati ya Kristo na Kanisa ndio maana Mt. Sipriano hasiti kutusaidia kutambua kuwa; “Kama hatuna Kanisa kama mama, hatuwezi kuwa na Mungu kama Baba.”


Imani iliyo hai
    Imani ambayo mwanzo wake ni Mungu mwenyewe, inapaswa kuwa hai na kwa hulka yake, kila kilicho na uhai kinakua. Mitume walipoyasikia mafundisho ya Yesu aliyeonya juu ya watu kuwa chanzo cha makwazo, Mitume wanaomba kuongezewa imani: “Bwana, tuongezee imani” (Lk 17:5). Mahali pengine tunakutana ya Yesu anayemponya yule kijana mwenye pepo. Pamoja na imani ya baba wa kijana huyu, bado alimwambia Yesu, “ukiweza neno lolote, utuhurumie” (Mk 9:22). Yesu anamjibu akisema: “Yote yawezekana kwake aaminiye” (Mk 9:23). Baba wa kijana anamalizia kwa kusema: “Naamini, nisaidie kutoamini kwangu” (Mk 9:24). Haya yalikuwa baadhi ya matukio katika Injili ambayo yanatufunulia ukweli kwamba, imani kwa asili yake inakua na inakua vema kama inakuzwa kwa msaada wa neema ya Kristo.


    Inapotokea kwamba kuna kutetereka katika makuzi ya imani ni wajibu wetu kukumbushana na kuhimizana, ili tuweze kuamka na kusimama tena katika imani. Huu ni mwaliko wa kurudi tena kwenye misingi ya imani na kujipima ili kuona kama maisha yetu bado yamesimama katika msingi wa imani au tumeanza kupotoka. Mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho anawapa changamoto akisema: “Jijaribuni wenyewe kwamba mmekua katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu?” (2Kor 13:5). Mtume Paulo anawataka wajipime kuona ni kwa kiasi gani na ni kwa namna gani waamini wa Korintho wamekua katika imani. Wakati kwa upande mmoja imani hujaribiwa na Mungu, kwa upande mwingine Mtume Paulo anatushauri tujipe nafasi za kujijaribu wenyewe ili tuone kama tunakua au tunadumaa katika imani. Zipo namna nyingi za kujijaribu wenyewe katika imani, lakini njia ya uhakika kabisa ya kujipima ni kuangalia ni kwa namna gani tunakua katika fadhila zile mbili zingine za kimungu; yaani matumaini na mapendo.

Imani hai: dhihirisho la matumaini na upendo
    Imani ya kweli inajidhihirisha katika matumaini na upendo. Fadhila hizi tatu za kimungu haziachani (Rej. 1Kor 13:13). Upendo, kama anavyoandika Mt. Agostino, kwa kawaida unatanguliwa na imani: “Upendo kwa Mungu na kwa jirani utatoka wapi bila imani? Anawezaje mtu kumpenda Mungu asiyemwamini?” Imani ni ufunguo unaotuingiza katika mji wa Mungu, mji ambao wale wanaoishi ndani yake, wanatembea kwa miguu ya matumaini na upendo. Imani ya kweli ni lazima ijidhihirishe kwa kukua katika matendo ya upendo (Rej. Yak 2:14-18 ). Huu ni ushuhuda wa upendo, unaojenga imani na kuikuza imani. “Imani inakua pale inapotiwa katika maisha kama uzoefu wa upendo uliopokelewa na pale inaposhirikishwa kwa wengine kama uzoefu wa neema na furaha. Inatufanya kuzaa matunda, kwa sababu inapanua ndani ya mioyo yetu matumaini na kutuwezesha kuwa na ushuhuda ulio hai: hakika, inafungua mioyo na akili za wale wanaosikiliza kuuitikia mwaliko wa Bwana wa kushikilia neno lake wa kuwa wafuasi wake.” Imani pia inajenga matumaini na matumaini ni dhihirisho la kile tunachokiamini. Kwa hiyo Mwaka wa Imani ni mwaliko pia wa kukua katika fadhila hizi za kimungu.

Changamoto mbali mbali hasa za mahusiano na watu wa Jumuiya nyingine za Kikristo na dini nyingine.

    Kama Wakristo Wakatoliki wa Tanzania tunaiishi imani yetu tukiwa katika jamii iliyo pia na watu wenye imani tofauti na imani yetu. Kati ya hawa wapo wanaoamini baadhi ya yale tunayoamini na wengine ambao hawaamini kabisa kile tunachokiamini. Pamoja na tofauti zetu za kiimani, Kanisa Katoliki linaamini katika uhuru wa kuabudu na linaheshimu watu wa dini na madhehebu yote. Kwa kuzingatia ukweli huo, Kanisa limejitahidi sana kuunda mazingira ya mazungumzano kati yake na wakristo wa madhehebu mengine na watu wa dini nyingine kwa lengo la kukuza mshikamano, kuheshimiana na kuelekeza nguvu zetu katika kudumisha utu wa binadamu na amani ya Taifa letu.
  1. Katika siku za karibuni yamejitokeza matukio yasiyopendeza na ya kusikitisha. Kashfa dhidi ya dini na madhehebu mengine zinazidi kuendelea na hali hiyo inaanza kuonekana kuwa ni utamaduni usio rasmi wa Taifa letu kwa sababu unafumbiwa macho. Yamekuwepo matukio ya kuchomwa moto kwa nyumba za ibada na baadhi ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini kutumika kuanzisha na kuendeleza malumbano, uchochezi, chokochoko na kashfa za kidini. Hali hii haijengi na ni kukosa heshima kwa imani za wengine. Kanisa linaamini kwa dhati kabisa kuwa, “Katika matumizi ya uhuru wowote, watu lazima waheshimu kanuni ya kimaadili ya uwajibikaji wa binafsi na wa kijamii.” Kama Kanisa Katoliki nchini tunawaomba waamini wetu msishawishike kutenda jambo lolote kinyume na maelekezo ya upendo wa kiinjili. Kuweni macho mkidumu katika sala. Kuweni wapole kama hua, lakini wenye busara kama nyoka (rej. Mt 10:16). Tunaomba msitumie muda wenu kuhubiri juu ya imani zisizowahusu. Jikiteni katika kuijua na kuiishi imani yetu kwa kina. Lakini pia tunaziomba mamlaka kuu kutoruhusu kujengeka utamaduni wa kusia mbegu za chuki na migongano inayoteteresha imani. Tusikubali kufika mahali ambapo matukio yasiyo ya kawaida yakaonekana kuwa ni ya kawaida, hasa yanapoendelea kutokea na nguvu za dola zikaonekana kuwa kimya au kuzidiwa nguvu.


Ushuhuda wa Imani

Familia
    Imani ya kweli inapimwa kupitia “afya” ya familia na ya jamii. Haya mawili yanategemeana. Imani isipojidhihirisha katika uhai wa familia, iliyo Kanisa la kwanza, la nyumbani na la msingi, itakuwa ni vigumu kujidhihirisha popote. Familia zetu zinazidi kuwa legelege kwa sababu hazichukuliwi tena kuwa eneo la malezi muhimu ya kiimani na ya kiutu. Malezi ya familia “yamebinafsishwa” katika tendo la kuamini kila mtu katika familia ana wajibu wa kujilea mwenyewe bila ya msaada wa mwingine kati ya wale wanaounda familia moja. Katika mazingira ya namna hii, dhana nzima ya familia inapotea na familia inapoteza fursa ya kuwa “shule ya imani”, ambamo wazazi na watoto, kwa pamoja, wanakua katika imani. Mwaliko huu wa Mtume Paulo kwa Kanisa la Korintho ni mwaliko kwanza kwa hili “Kanisa la nyumbani”. Tunazihimiza familia zote za Kikristo kuizingatia imani kwa dhati: Familia, “Simameni imara katika imani”! Ipelekeni nyumbani ile imani mliyoipokea kutoka kwa Mungu kupitia Kanisa lake. Humo mkaiishi na kuijengea mazingira ya kukua. Hili linapotekelezwa, familia itakuwa na uwezo wa kuipeleka imani katika jamii.


    “Familia inapata katika mpango wa Mungu Mwumbaji na Mkombozi sio tu utambulisho wake; yaani, yenyewe ni nini, bali pia utume wake; yaani, ni nini inachoweza na inachopaswa kufanya”. Familia zinapoutambua utambulisho wake na utume wake zinaweza kuiishi imani kwa namna bora zaidi. Huo unakua ndiyo mwanzo wa ushuhuda wa kikristo. Ndani ya familia panakuwa ni mahali unamozaliwa moyo wa huruma kwa wanyonge na wasiojiweza. Humo imani inakuwa ni jibu la kutatua hali za kutoelewana katika familia. Ni kwa namna hii tunaweza kupiga hatua ya kwanza katika kuboresha mazingira ya mahali tunamoishi, kwa sababu “familia ni mahali panapofaa pa kujifunzia na kuzoeshwa utamaduni wa msamaha, amani na upatanisho”. Kwa sababu hiyo wajibu wa malezi endelevu ya imani katika familia unapaswa kuwa wa kudumu. Kwa namna hii tunaweza kuanza kupiga hatua ya kwanza katika kupambana na maradhi hatari kama UKIMWI, kupambana na rushwa, uzembe, na tabia zote ambazo zina athari mbaya kwa makuzi ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Kwa njia ya imani familia zitapata furaha ya kweli inayojengwa kupitia fadhila za amani na upendo.




Kazini na katika Jumuiya
    Mwaliko wa kusimama imara katika imani hauishii kanisani na katika familia tu, ila unaanzia hapo na kutoka hapo mwaliko huu unatekelezwa popote tunapokwenda. “Kukiri kwa mdomo inaonesha kuwa imani inamaanisha ushuhuda na wajibu wa hadharani pia. Mkristo hatakiwi kamwe kufikiri kuwa imani ni tendo la faragha. Imani ni kuchagua kusimama na Bwana ili kuishi naye.” Kuipeleka imani katika jamii ni tendo la ushuhuda wa kikristo. Mtume Yohane anatufundisha kuwa ni kwa njia ya imani tu ndipo tunaweza kuushinda ulimwengu: “Na huku ndiko kuushinda ulimwengu: hiyo imani yetu” (1Yoh 5:4). Tendo la ushuhuda wa mkristo linalojidhihirisha kwa njia ya imani halina maana ya kujaribu kuwalazimisha watu wengine kuwa wakristo, bali ni kutia katika matendo misingi ya upendo, haki, amani na maelewano kama Kristo anavyotuagiza, na kwa namna hii tunatakatifuza maeneo ya kazi zetu za kila siku na jumuiya zetu. Huku ndiko kuwa chumvi na nuru ya ulimwengu. Na Baba Mtakatifu Benedikto XVI anatuhimiza akisema: “Hatuwezi kukubali chumvi ipoteze ladha au mwanga ubaki umefichwa (rej. Mt 5:13-16).”
  1. Imani ya kweli, ambayo inajidhihirisha katika tendo la waamini kujitoa kama vyombo safi ambavyo Mungu anavitumia kuiumba upya na kuitakatifuza dunia, ni chachu ya kweli kwa mwanadamu na kwa ulimwengu. “Je, si kazi ya Kanisa kutoa mwanga wa Kristo katika kila kipindi cha historia? Si kazi yake kufanya uso wa Kristo ung’are pia mbele ya vizazi vya hii milenia mpya?” Basi, wakati huu wa Kwaresima ni wakati wa kuifanya upya imani yetu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, hasa Sakramenti ya Upatanisho. Vile vile, huu ni wakati wa kufufua matendo ya huruma na upendo na kuyafanya kuwa endelevu katika maisha yetu.

  2. Kanisa hapa nchini linatambua “mchango mkubwa ambao wanawake na wanaume walitoa na kusaidia kukua na kuendelea kwa jumuiya kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.” Baba Mtakatifu Mwenyeheri Yohane Paulo II atabaki kwetu kuwa ni tunda la utakatifu uliojidhirisha katika uaminifu wake kwa Kristo aliyemtanganza na kumtumikia. Maisha yake ya sala, uvumilivu, uongozi wake shupavu na msimamo wake usiotetereka katika kuitafuta na kuikazia macho sura ya Yesu, imemfanya kuwa shahidi wa imani anayepaswa kuwa mfano wa kuigwa. Wapo pia Watanzania wenzetu ambao maisha yao yalikuwa ni kielelezo cha imani inayojidhihirisha katika matendo. Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Nyerere, mwanasiasa mweledi, akiongozwa na dhamiri ya kikristo, ni mmoja wa wakristo waliotukuka katika maisha ya uadilifu wa kisiasa na kiutu. Mtumishi wa Mungu Sr. Bernadetta Mbawala wa shirika la masista Wabenediktini wa Mt. Agnes Chipole, naye alifanikiwa kuitafsiri imani katika maisha yake na hivi akaishi maisha ya upendo unaobubujika kutoka katika imani kwa Mungu na kwa Kanisa. Wakumbukeni hawa na wengine wengi walioishi miongoni mwetu wakimshuhudia Kristo kwa maisha yao, tena, “iigeni imani yao” (Ebr 13:7).



SURA YA NNE


MATUKIO MUHIMU

Miaka 150 tangu Wamisionari wa Kwanza walipotua visiwani Zanzibar
    Tunapotafakari mwaliko huu wa kusimama imara katika imani, historia inatukumbusha pia kuwa miaka takribani 150 iliyopita, imani hii tunayoiishi na kuiadhimisha ilitufikia kupitia visiwa vya Zanzibar. Yesu Kristo, aliye Mlango wa Imani, ni Njia vilevile inayotuelekeza na kutuongoza kwenye Uzima. Yote huanzia na kuishia kwake. Hata hivyo, Yeye aliye Njia na Mlango hutufungulia “njia” nyingine nyingi na “milango” mingine mingi inayotuelekeza kwake Yeye aliye utimilifu wa yote.
  1. Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu walipofika Zanzibar, mnamo mwaka 1860, hawakuishia hapo, bali wakitokea katika visiwa hivyo waliivusha mbegu ya imani hadi Tanganyika ya wakati huo na kuanza kuipanda katika mji wa Bagamoyo mnamo mwaka 1868. Mbegu hii ya imani iliendelea kuchipuka na kukua kupitia wamisionari wa mashirika mbali mbali; wakiwemo Wamisionari wa Afrika, Wabenediktini wa Mt. Ottilia na wengine wengi baada yao, ambao wote katika ujumla wao walikuja kwa lengo la kuinjilisha na kuhakikisha kuwa imani inaota mizizi yake katika maeneo ya nchi yetu. Wamisionari hawa pamoja na kuwa na karama mbali mbali, waliunganishwa na lengo moja ambalo lilikuwa ni kutangaza habari njema. Kwa sababu hiyo, kila kundi, kwa wakati wake na kwa namna yake limetoa mchango wake uliotukuka, ama katika kupanda au katika kumwagilia mbegu na mche wa imani, na Mungu ameendelea kuukuza huu mche wa Imani (Rej. 1Kor 3:6).



    Kumbukumbu hii inapaswa kuijaza mioyo yetu shukrani kwa Mungu aliyetupatia zawadi ya imani, zawadi iliyo kuu ya upendo wake. Shukrani yetu inapaswa, hata hivyo, kuvuka mipaka ya kubaki katika maneno tu na kuwa tendo la kudumu kiaminifu katika imani, kuifanya imani kuwa dira inayoongoza kila tendo la maisha yetu ya kila siku na kuhakikisha kuwa imani tuliyoipokea inazidi kustawi na kushamiri.

Mwaka wa Imani na Mkutano wa Kawaida wa Kumi na Tatu wa Sinodi ya Maaskofu

    Mwezi Oktoba 2012, kuanzia tarehe 7 hadi 28, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alikutana Roma na Maaskofu kutoka ulimwenguni kote kwa ajili ya Sinodi ya 13 ya Kawaida ya Maaskofu iliyokuwa na mada: “Uinjlishaji Mpya kwa ajili ya Kueneza Imani ya Kikristo”. Sinodi hii ilikuwa na lengo la kuzindua programu ya Uinjlishaji Mpya. Sinodi ilitafakari kwa kina njia mpya na muafaka zitakazolisaidia Kanisa na wanakanisa wote kuifanya imani kuwa ni sehemu ya uhalisia wa maisha ya kila siku ya waamini, kwa kuiishi kwa ari inayokuwa na kukomaa katika maneno, matendo na mienendo ya maisha.


    Tarehe 11 Oktoba 2012, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alizindua Mwaka wa Imani ambao utafikia kilele chake wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme tarehe 24 Novemba 2013. Lengo msingi la Mwaka wa Imani limewekwa bayana na Baba Mtakatifu katika hati yake Porta Fidei (Mlango wa Imani).
  1. Mwaka wa Imani ni mwaliko wa kurudia upya ungamo la imani na kulitia katika matendo ya maisha ya kila siku. Ni wakati wa kupokea kwa shukrani zawadi ya imani ambayo kwa ubatizo mlango wa mahusiano ya kina na Mungu unafunguliwa. “‘Mlango wa Imani’ (Mdo 14:27) daima umefunguliwa kwa ajili yetu na kutuongoza katika muungano na Mungu na kutuingiza ndani ya Kanisa lake. Inawezekana kuvuka kizingiti hicho pale neno la Mungu linapotangazwa na moyo unapojiruhusu kuundwa kwa kugeuzwa na neema. Kupita katika mlango huo ni kuanza safari itakayodumu kwa maisha yote.” Safari hii kwa wakati wa sasa inabeba pia mwaliko wa Uinjilishaji Mpya kwa sababu zipo dalili na maelekeo makubwa ya Wakristo kusahau au/na kuzembea maisha ya imani.

  2. Imani ya Kanisa sio tu matamko mbalimbali ya Kanisa, bali ni uhusiano hai na Yesu Kristo, aliye Kichwa cha Kanisa, na uhusiano na Mwili wake, yaani Kanisa. Tunachokiamini ni Ukweli uliofunuliwa kwetu na Yule ambaye ndani yake tunaamini, Yesu Kristo, Ukweli unaoendelezwa na Kanisa chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Kwa hivi, Kanisa lina wajibu huo wa kuiendeleza imani kwa kuwa, “Kazi ya kueneza Injili ni wajibu na ndio utume halisi wa Kanisa.”Njia ya kutekeleza wajibu huo ni “kutweka mpaka kilindini”, ambako ndiko dhamana ya wakati huu wa kihistoria kwa Kanisa iliko. Hatua hii ya matumaini italiwezesha Kanisa kuchukua hatua mpya mbele katika historia.



SURA YA TANO

IMANI KATIKA MAISHA YA KISIASA

    Tunapoisoma Barua kwa Dionyeto, moja ya barua za kikristo za karne ya pili, tunaambiwa ifuatavyo juu ya wakristo wa Kanisa la mwanzo: “Wanashiriki kila jambo kama raia… Wanatii sheria zilizowekwa na maisha yao ya uadilifu wanayaishi vizuri kupita madai ya sheria.” Anaendelea kusema pia, “kama roho ilivyo kwa mwili ndivyo wakristo walivyo kwa dunia.” Ushiriki wa waamini katika shughuli za jamii na siasa ni sehemu ya wajibu wa kiimani. Lengo la ushiriki huu ni kusaidia kujenga jamii iliyo bora zaidi, kwa sababu, “ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote.” Kwa kutekeleza wajibu huu wakristo wanapata fursa ya kuwa “mwanga na nuru” kwa ulimwengu (Mt 5:14) na kuwa “wahudumu wa hekima ya kikristo” katika jamii inayowazunguka.


Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

    Taifa letu lipo katika kipindi mahsusi cha historia. Katiba yetu inaandikwa upya. Uamuzi huu ni matokeo ya tafakari ya kina iliyobaini kuwa kuna uhitaji wa sisi kama taifa kuwa na Katiba inayokwenda na wakati na zaidi sana Katiba itakayotoa dira ya taifa kwa kipindi kirefu kijacho. Tunapenda kuwaalika wakristo wote na watu wote wenye mapenzi mema kutekeleza zoezi hili kwa umakini na uadilifu mkubwa, tukitambua kuwa suala hili la Katiba ni wajibu uliotukuka ambao raia wanaushiriki katika maisha yao. Wakati dini, makabila na hali zetu zinatutofautisha, Katiba ya nchi inabaki kuwa ni chombo kinachotuunganisha katika kuwa na haki sawa na wajibu sawa, ndani ya nchi yetu. Imani zetu hazitunyang’anyi na wala hazilengi kutufanya kupoteza utaifa wetu bali zinatusaidia kuijenga misingi ya mshikamano, amani na uadilifu ambayo dini zetu zinapaswa kutufundisha kuitekeleza.


    Wajibu huu kwetu ni mkubwa kwa sababu tunapoutekeleza tunachangia kujenga misingi imara ya Taifa, nalo ni jambo lililo muhimu sana. Mzaburi anatukumbusha anapouliza: “Kama misingi ikiharibiwa mtu mwadilifu atafanya nini?” (Zab 11:3). Misingi yoyote ile, iwe ya imani au ya Taifa inapoharibiwa hata mtu mwadilifu anatetereka. Fursa kama hii ya kuipitia upya Katiba inakuwa ni wajibu wenye msukumo wa dhamiri kutoa mchango wetu ili hatimaye tuwe na Katiba bora. Katiba isiyoheshimiwa inaporwa uhai wake. Tungependa kuona sisi tulio Wakristo, tunaosukumwa na Amri Kuu ya upendo, kwa Mungu na kwa jirani (Rej. Mt 22:36-40), tuwe msitari wa mbele katika kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za nchi zinazotuongoza.


    Zoezi la kutoa maoni ya Katiba lina hatua mbalimbali. Tume imekwishaanza kazi yake. Tunapoendelea na zoezi hili ni vema “tujiulize kama tunaamini kweli Mafundisho ya Mungu na tuko tayari kuwajibika mbele ya Mungu na mbele ya jamii juu ya maamuzi na vipaumbele vyetu? Je, tunaamini kweli ujumbe wa Kristo kuwa Mungu ni Baba wa watu wote ambao huunda familia ya wanadamu?” Ni kwa sababu hiyo, tunapendekeza Katiba yetu itamke wazi kuwa hakuna mtu yeyote aliye juu ya Katiba. Iwe ni Katiba inayoweza kumhoji kila mtu, wakati wowote na aliye katika nafasi yoyote. Iwe ni Katiba inayolinda na kutetea uhai na hadhi ya mtu tangu kutungwa mimba mpaka kufa kifo cha kawaida. Katiba itamke wazi pia juu ya familia inayoundwa na baba, mama na watoto. Zaidi sana, tungependa Katiba ifufue roho halisi ya uraia, yaani uzalendo wa kitanzania. Katiba isipotafsirika kama dhamiri ya wajibu wa kizalendo itakuwa imeporwa uhai wake. Katiba iwe zao la uadilifu na ikabidhiwe kwa utekelezaji wake kwa wale ambao, si zaidi kwa maneno bali kwa matendo, wanajipambanua kuwa waadilifu kwa kila hali. Katiba itakosa “uhai” wake kama wale waliopewa wajibu wa kuilinda, kuitetea na kuisimamia hawafanyi hivyo.


    Lakini ikumbukwe wazi kwamba wajibu wa kuilinda na kuitetea Katiba, kwa nafasi ya kwanza, ni wajibu wa kila raia. Katiba ni mali ya wananchi. Wale waliopewa dhamana ya kuilinda na kuisimamia si wamiliki wa Katiba bali mawakili tu wanaopaswa kukumbuka siku zote kuwa wameajiriwa na wananchi kuisimamia Katiba na si kuitawala Katiba.


    Hatuna budi kutafakari na kujiuliza ni kwa nini, pamoja na kuwa na Katiba na sheria unaendelea kutawala utamaduni wa “kujichukulia sheria mkononi” iwe ni kwa wananchi wa kawaida na hata kwa wale waliopewa dhamana ya kuilinda, kuitetea na kuisimamia Katiba. Raia wanapojichukulia sheria mkononi ni dhihirisho la kutokuwa na imani na wale waliopewa dhamana ya kuisimamia sheria. Na pale inapotokea wale waliopewa dhamana ya kuilinda na kuitetea wanajichukulia sheria mkononi kwa kuipindisha, kwa kutoitetea na kuilinda hilo ni dhihirisho la kutokuamini kwa dhati kile walichotamka mbele ya Mungu na wananchi. Tunarudia kusema kwamba, tunapaswa kuunda na kujenga utamaduni wa kuheshimu Katiba, sheria na taratibu zinazotuongoza.


HITIMISHO
    Tunapenda kuhitimisha ujumbe huu wa Kwaresima ya mwaka huu tukizidi kuwatia moyo wa kudumu imara katika safari ya imani, “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu” (Ebr 12:2). Tusikubali kupoteza imani yetu. Hata pale mwendo katika safari ya imani unapogeuka kuwa mgumu, simameni imara “mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake” (Kol 1:23).
  1. Kipindi cha Kwaresima, kama ulivyo pia Mwaka wa Imani, ni safari kuuelekea Ufufuko wa Bwana, ambao ni mlango wetu sisi wa kuingia katika maisha mapya ya uzima wa milele. Kumshuhudia Kristo Mfufuka ni kuishi katika upya wa maisha. Na kwa kuwa tunazidi kupoteza tunu bora za kuishi katika upya wa maisha, hatuna budi kujikita katika Uinjilishaji Mpya wenye lengo la kutufanya upya katika wajibu wetu wa Kikristo na kusaidia kuufanya ulimwengu kuwa mahali ambapo Mungu anapewa utukufu na sifa. Tunawaalika pia kushiriki kikamilifu kalenda na mipango iliyopendekezwa na Kanisa la Ulimwengu kwa Baraza la Maaskofu, Majimbo, Parokia, Vigango na Vyama vya Kitume. Msiogope. Hatuko peke yetu. Simameni imara katika imani. Pamoja nasi katika safari hii ya imani tunaye Mama Mbarikiwa Bikira Maria. Huyu ni Mama wa Imani, aliyepata heri kwa sababu alisadiki na kwa kusadiki kwake yakatimizwa aliyoambiwa na Bwana (Rej. Lk 1:45). Tunawatakieni safari njema ya imani katika mfungo wenu wa Kwaresima. Safari hii imfikishe kila mmoja wetu kwenye furaha ya Pasaka ya Ufufuko.



Ni sisi Maaskofu wenu,
    Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam
    Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Iringa
    Mhashamu Askofu Mkuu Norbert Mtega, Songea
    Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu, Arusha
    Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora
    Mhashamu Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi – Mwanza
    Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro
    Mhashamu Askofu Gabriel Mmole, Mtwara
    Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
    Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
    Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
    Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
    Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar
    Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga
    Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
    Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba
    Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba
    Mhashamu Askofu Damian Dallu, Geita
    Mhashamu Askofu Ludovick Minde, ALCP/OSS, Kahama
    Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe
    Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi
    Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Mbulu
    Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma
    Mhashamu Askofu Isaack Amani, Moshi
    Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga
    Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp,Same
    Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
    Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam
    Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda
    Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga – Dodoma
    Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa – Kondoa
    Mhashamu Askofu John Ndimbo - Mbinga










All the contents on this site are copyrighted ©.