2013-03-07 08:09:09

Mikutano ya Makardinali ni fursa ya kusali, kutafakari na kushirikishana mang'amuzi na vipaumbele vya Kanisa


Makardinali wanaendelea kusali, kutafakari na kushirikishana mang'amuzi, matatizo, changamoto, fursa za vipaumbele kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, wakati huu wanapojiandaa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kung'atuka kutoka madarakani na sasa anaendelea kulisindikiza Kanisa kwa njia ya sala na tafakari ya kina.

Historia ya Kanisa inaonesha kwamba, Kardinali Walter Kasper, aliyetimiza miaka 80 tangu alipozaliwa mapema juma hili, ataendelea kuwamo kwenye orodha ya Makardinali wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura na kwamba, ndiye Kardinali mwenye umri mkubwa kupita wote aliyebahatika kupata dhamana hii katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii inatokana na ufafanuzi wa kisheria uliotolewa kwamba, haki ya Kardinali kupiga au kupigiwa kura kutokana na umri unaanza pale kiti cha ukulu wa Mtakatifu Petro kinapokuwa wazi.

Makardinali wanaendelea kuchambua kwa kina na mapana kuhusu changamoto zilizobainishwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu dhamana ya Uinjilishaji Mpya, Kanisa na Ulimwengu, uhusiano kati ya Mabaraza ya Kipapa na Maaskofu, bila kusahau matarajio ya Makardinali kuhusu wasifu wa Papa Mpya, atakayeliwezesha Kanisa kuendeleza na kudumisha utawala bora.

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Makardinali waliotoka Marekani walikuwa wamejiwekea utaratibu wa kukutana na kubadilishana mawazo na Waandishi wa Habari kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanalofuatilia mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya hapa Vatican kwamba, utaratibu huo kwa sasa umefutwa.

Anakumbusha kwamba, mikutano ya Makardinali inayoendelea kwa sasa si Sinodi wala Makongamano ambayo viongozi wa Kanisa wanaweza kushirikisha mawazo na maoni yao au yale yaliyojiri katika mikutano hiyo! Mikutano ya Makardinali kwa sasa ni fursa ya kusali, kutafakari na kupembua vipaumbele vya Kanisa, ili hatimaye, kuwawezesha Makardinali kufanya maamuzi ya busara wakiongozwa na Roho Mtakatifu, kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa la Kristo.

Hii ni mikutano ya faragha anasema Padre Federico Lombardi, ili kutoa fursa kwa Makardinali kuwa huru kushirikisha mawazo yao kwa Makardinali wengine. Waamini na watu wenye mapenzi mema, wanaalikwa kwa namna ya pekee kuvuta subira, kuhusu tarehe ya kuanza uchaguzi wa Papa Mpya. Kwa sasa mwelekeo ni kwamba, Makardinali wanataka kupata nafasi pana zaidi kwa ajili ya kusali, kutafakari na kupembua hali ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na changamoto nyingi. Kutokana na mantiki hii, hakuna haraka ya kupanga tarehe kwa sasa, lakini wakati ukiwadia waamini watajulishwa.

Padre Federico Lombardi anasema kwamba, Pete ya Mvuvi iliyokuwa inatumiwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita wakati wa uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, imekwaruzwa na haiwezi tena kutumika na kwamba, itahifadhiwa.







All the contents on this site are copyrighted ©.