2013-03-07 08:24:36

Makardinali wanasali kwa ajili ya Kanisa!


Makardinali wanaoendelea na mchakato wa kumchagua Papa Mpya baada ya mkutano wao Jumatano, tarehe 6 Machi 2013, jioni walikusanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa. Kwa namna ya pekee, wakati huu Makardinali wanajiaminisha mikononi mwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa kwa kusali na kutafakari Rozari Takatifu, muhtasari wa maisha na utume wa Yesu. Makardinali pamoja na waamini wanaokusanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wanasali kwa lugha ya Kiitalia na Kilatini.

Baada ya Rozari Takatifu, Makardinali walipata fursa ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na kusali katika ukimya, kama njia ya kuzungumza na Yesu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na baadaye, walisali Masifu ya Jioni na Baraka ya Ekaristi Takatifu. Ibada hii imeongozwa na Kardinali Angelo Comastri, Kasisi mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Huu ndio utaratibu utakaofuatwa wakati huu Makardinali wanapoelekea kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro.







All the contents on this site are copyrighted ©.