Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kimataifa, tarehe 8 Machi 2013
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, inayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe 8
Machi ni fursa ya kufanya tafakari ya kina ili kuangalia matukio yanayopelekea unyanyasaji
na dhuluma dhidi ya wanawake, ili kuibua mbinu mkakati wa kuwa na kesho iliyo bora
zaidi kwa wanawake wengi zaidi. Kuna wanawake wanaoendelea kunyanyasika kiasi hata
cha kuamua kutema zawadi ya uhai ili kuficha aibu yao.
Katibu mkuu wa Umoja
wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon katika ujumbe wake kwa Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa
kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi, anawaalika watu kuondokana na mambo yanayopelekea
nyanyaso na dhuluma kwa wanawake, kwa kujali na kuthamini utu na heshima yao; wahusika
wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, ili kukomesha tabia hii inayoendelea
kukua na kupanuka katika Jamii nyingi.
Katika maeneo ambayo kuna vita na migogoro
ya kivita, unyanyasaji wa kijinsia umekuwa ni silaha nyingine inayotumiwa na wanajeshi
ili kuwadhalilisha maadui, lakini wanashindwa kutambua kwamba, wanadhalilisha utu
na heshima ya mtu. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anapenda kuwahakikishia wanawake
wanaoteseka, wanaodhulumiwa na kunyanyasika kwamba, Jumuiya ya Kimataifa iko pamoja
nao.
Umoja wa Mataifa unataka kuwasaidia kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika
kupinga udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na kwamba, wanawake watambuliwe
na kuheshimiwa kama wadau wakuu wa ujenzi wa amani katika Jamii. Ikumbukwe kwamba,
wanawake wanayo haki ya kuishi bila kunyanyasika.