Boresheni hali ya wanawake katika nchi zinazoendelea ili wachangie katika sekta ya
maendeleo!
Katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kimataifa inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo
tarehe 8 Machi, Umoja wa Mataifa unaendelea kuzihamasisha Serikali na wadau mbali
mbali kuongeza juhudi katika kuwajengea uwezo wanawake kwa njia ya elimu ili kupambana
na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha yao ya kila siku. Juhudi
hizi hazina budi kwenda sambamba pia na harakati za kupambana na umaskini, njaa na
lishe duni.
Haya yamo kwenye taarifa ya haki msingi za binadamu iliyotolewa
hivi karibuni na Baraza la Haki Msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Shughuli za
uzalishaji katika sekta ya kilimo hasa kwa ajili ya chakula cha kifamilia inafanywa
kwa sehemu kubwa na wanawake, kwani wanaume wengi wako mijini wakitafuta fursa za
ajira. Licha ya ukweli kwamba, wanawake ndio wazalishaji wakuu katika sekta ya kilimo,
lakini bado wanatumia nyenzo duni na wengi wao hawana elimu ya kutosha kuongeza tija
na uzalishaji.
Kuna haja pia kwa Serikali kufanya maboresho katika sheria
kandamizi dhidi ya wanawake pamoja na kutoa huduma za msingi kwa wanawake na familia
zao. Wanawake wanahitaji kupata maji safi na salama, nishati ya uhakika, huduma bora
za afya na elimu kwa ajili yao wenyewe na watoto wao. Baraza la Haki Msingi za Binadamu
la Umoja wa Mataifa linasema kwamba, wanawake wakiwezeshwa kikamilifu wanaweza kuchangia
kwa kiasi kikubwa uzalishaji katika sekta ya kilimo na mapambano dhidi ya baa la njaa
duniani.