2013-03-06 09:13:42

Venezuela yakumbwa na msiba wa kitaifa! Mazishi kufanyika Ijumaa, tarehe 8 Machi 2013


Rais Hugo Rafael Chàves Friars wa Venezuela amefariki dunia kutokana na kushambuliwa na ugonjwa wa mapafu uliomfanya kushindwa kupumua na hatimaye, kufariki dunia, tarehe 5 Machi 2013. Rais Chavès aliyekuwa na umri wa miaka 58, hali yake ilianza kudhohofu katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita na hivyo kulazimika kulazwa kwenye Hospitali ya Kijeshi nchini mwake. Serikali ya Venezuela imetangaza siku 7 za maombolezo na anatarajiwa kuzikwa Ijumaa tarehe 8 Machi 2013.

Itakumbukwa kwamba, Rais Hugo Chàves alifanyiwa upasuaji mkubwa nchini Cuba, hapo Desemba 2012 baada ya kugundulika kwamba, alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa saratani. Katika kipindi cha miaka miwili amefanyiwa operesheni kubwa nne.

Wananchi wa Venezuela wanaomboleza kutokana na kifo cha Rais Chàves aliyeleta mapinduzi makubwa nchini mwake, kwa kuhimiza demokrasia shirikishi iliyowafanya wananchi wa Venezuela kutoka kifua mbele. Akabadilisha katiba kwa Rais kuweza kuongoza kwa kipindi cha miaka sita na kwamba, Rais angeweza pia kuongoza kwa awamu mbili tu, ili kutoa nafasi kwa wananchi wengine wa Venezuela kuendeleza libeneke la maendeleo yao, lakini wapinzani wake hawakufurahia mwelekeo huu.

Rais Chàves anakumbukwa na wengi kama kiongozi aliyekuwa na karama ya uongozi na mvuto mkubwa kwa wananchi wake. Ni kiongozi aliyediriki kufanya maamuzi machungu kwa ajili ya mafao ya watu wake hasa katika uwanja wa mawasiliano ya kijamii, lakini bado walimlaumu kwa kuwanyima watu uhuru wa kujieleza!

Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela, katika barua yao ya kichungaji ya Mwaka 2007 kwa kuonesha jinsi ambavyo Serikali ilishindwa kutatua matatizo ya wananchi wake, kiasi kwamba, wengi walikuwa wanaogelea katika umaskini, ukosefu wa fursa za ajira, rushwa na ufisadi; kukithiri kwa vitendo vya jinai pamoja na kukumbatia utamaduni wa kifo. Vitendo vya utekaji nyara; kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja matumizi ya fedha chafu.

Rais Chàves alikuwa na msimamo mkali wa sera na siasa za nchi za nje, kiasi kwamba, ni mtu ambaye "hakuweza kula sahani moja" na Washington, DC.Alihimiza ushirikiano kati ya Nchi zinazoendelea, hasa kutoka Amerika ya Kusini, ili kuweza kupambana na changamoto zilizokuwa zinawakabili. Alikuwa na uhusiano wa pekee na Iran, Korea ya Kusini na Ukrain.

Rais Chàves umaarufu wake ulianza kupungua kunako mwaka 2012 alipoanza kubanwa na ugonjwa, hali ya uchumi ikadhohofu kiasi kwamba, mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma ukapanda hadi kufikia asilimia 30%; deni la ndani na nje likaongezeka maradufu; ulinzi na usalama vikaanza kuwa mashakani. Miaka 13 ya uongozi wake, ukaanza kuchakaa kama kanga! Wananchi wa Venezuela wanamlilia kwa mengi!

Wananchi wa Cuba wanaomboleza pia msiba wa Rais Chàves ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Cuba hasa katika masuala ya biashara ya mafuta kwa Cuba na Cuba ilikuwa inatoa nafasi ya Madaktari wake kufanya kazi nchini Venezuela pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa wanafunzi kutoka Venezuela. Rais Barack Obama wa Marekani anasema wataendelea kushirikiana na wananchi wa Venezuela ili kudumisha misingi ya demokrasia, utawala wa sheria na utekelezaji wa haki msingi za binadamu.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anasema Rais Chàves alikuwa ni kiongozi aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatetea wanyonge, atakumbukwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kuleta amani na utulivu katika nchi za Amerika ya Kusini.







All the contents on this site are copyrighted ©.