Makardinali wanasema, ndani ya Kanisa hakuna haraka ya uchaguzi!
Kardinali Antonio Maria VegliĆ² anasema, Makardinali hawana haraka ya kukimbilia kufanya
uchaguzi wa Papa Mpya, bado wanapenda kutumia fursa hii ili kusali, kutafakari pamoja
na kujadili kuhusu hali ya maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia
ya tatu ya Ukristo, matatizo, fursa na changamoto zilizopo, ili kuweza kujipanga vizuri
zaidi.
Makardinali waliotoka nje ya Roma wanapenda kufahamu kwa undani zaidi
kashfa zilizojitokeza kwa kuvujisha siri za Vatican, kwa kile ambacho kwa wengi sasa
kinajulikana kama "Vatileak.". Hii ni haki na wajibu wao kwani wao ni viongozi waandamizi
wa Kanisa.
Kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kulikabili Kanisa
kwa sasa, Kanisa linahitaji kuwa na Baba Mtakatifu mwenye utakatifu wa maisha, ili
uweze kuwa ni mfano na kielelezo cha kuigwa na wengine; awe ni mtu mwenye hekima na
busara, fadhila zitakazomsaidia kutekeleza maamuzi yake msingi katika wajibu wa: kufundisha,
kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu.
Ikiwezekana awe na umri utakaomwezesha
pia kukabiliana na changamoto za safari na maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro; akiwa na afya njema, ni sifa ya ziada, lakini yote haya Makardinali wanamwachia
Roho Mtakatifu ili awasaidie na kuwaongoza katika uchaguzi wa Papa Mpya.
Ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia sanjari na mapambazuko ya Millenia
ya tatu ya Ukristo, yanahitaji kiongozi ambaye atakuwa mkweli na shahidi wa uinjilishaji
Mpya ili kwa njia ya ushuhuda wa maneno na matendo yake, aweze pia kukabiliana na
changamoto za maadili yanayotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika tiba
na afya ya mwanadamu.
Mahali anapotoka mtu kijiografia si tatizo la Kanisa,
wala Makardinali hawaangalii rangi ya mtu haya ni matatizo yanayopigiwa debe na vyombo
vya habari kwa masilahi yao binafsi. Makardinali wanasema, hakuna haraka ya kufanya
haraka ya uchaguzi wa Papa Mpya, kwani wanataka kufanya upembuzi wa kina kuhusu maisha
na utume wa Kanisa, ili kutoa dira na mwelekeo sahihi kwa Kanisa kwa siku za usoni,
ili kujenga umoja, upendo na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.