2013-03-06 08:09:55

Katiba ya nchi inapaswa kuheshimiwa na wote kwani ni mhimili wa umoja na mshikamano wa kitaifa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo limemwandikia barua Rais Joseph Kabila wa DRC kwa kusisitiza kwamba, kwa vile Katiba ya nchi ni sheria mama inapaswa kulindwa na kuheshimiwa na wananchi wote wa DRC bila ubaguzi kwani hii ni nguzo muhimu ya umoja na mshikamano wa kitaifa.

Hivi karibuni, serikali iliamua kufanya marekebisho kwenye Ibara ya 220 ya Katiba ya nchi, jambo ambalo linapingwa na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC. Maaskofu wanasema, Ibara hii ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa DRC, kumbe kuna haja kwa wananchi kufahamu vyema Katiba, ili kuisimamia, kuilinda na kuitekeleza.

Maaskofu Katoliki DRC katika barua yao kwa Rais Kabila wamegusia pia hali ya kisiasa, kiuchumi na maendeleo ya kijamii. Wanampongeza kwa kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kisiasa yanayopania kuleta amani na utulivu kutokana na kinzani zilizojitokeza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini DRC, hapo Novemba 2011.

Kuhusu masuala ya uchumi na maendeleo Maaskofu wanabainisha kwamba, kuna matumizi mabaya ya rasilimali ya nchi, kwani wanaofaidika ni watu wachache wakati mamillioni ya wananchi wa DRC bado wanaendelea kuogelea katika dimbwi la ujinga, umaskini na maradhi. Ukata na hali ngumu ya maisha ya wananchi wa DRC unawatia uchungu kama viongozi wa kidini. Kuna haja ya kubadilisha mwelekeo huu ili rasilimali ya nchi iweze kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi.

Ili kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu, Maaskofu Katoliki DRC wanasema, kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa mahakama na kwenye vikosi vya ulinzi na usalama. Umefika wakati muafaka kwa Serikali na wananchi kwa ujumla kusimama kidete kupambana kufa na kupona na rushwa na ufisadi. Serikali ianzishe mikakati itakayowezesha amani na utulivu kutawala tena eneo la Mashariki ya DRC, ambalo wananchi wake wanaishi kwa hofu na vitisho kutokana na uwepo wa makundi yenye silaha.







All the contents on this site are copyrighted ©.