2013-03-05 13:45:37

Vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanachangamotishwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu na jambo lolote linalokwenda kinyume cha utu wa mwanadamu linapingana na mpango wa Mungu. Maaskofu wameyasema hayo mara baada ya kuhitimisha Kongamano la Kimataifa lililokuwa linajadili pamoja na mambo mengine kuhusu "imani na utu wa binadamu".

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linabainisha kwamba, makosa yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu ni pamoja na: mauaji, utoaji mimba, kifo laini, kujinyonga, ukeketaji, mauaji ya kimbari, madhulumu, maisha duni, vifungo vya watu wasiokuwa na hatia, utumwa, ukahaba, biashara haramu ya binadamu pamoja na hali na mazingira duni ya kazi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, nchini mwao wanakabiliwa na mambo yanayohatarisha utu na heshima ya binadamu. Mambo haya ni pamoja na ukosefu wa utawala bora; ukosefu wa ulinzi na usalama; rushwa na ufisadi; mmong'onyoko wa maadili na kanuni bora za uongozi; udhalilishaji wa haki msingi za raia wa Nigeria kwa misingi ya kikabila, kidini, kijinsia na kijiografia na mahali anapotoka mtu.

Haya ni baadhi ya mambo yanayohatarisha na kuendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Vitendo vya kigaidi vinavyotekelezwa na kikundi cha Boko Haram na makundi yenye silaha ni hatari kwa heshima na utu wa mwanadamu. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria lina laani mauaji yanayofanywa kwa misingi ya kidini; nchi ambayo kwa sasa uhuru wa kuabudu uko mashakani na unatolewa kwa baadhi ya wananchi tu jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika!







All the contents on this site are copyrighted ©.