2013-03-04 15:57:32

Kikao cha kwanza cha Makardinali- Vatican


Katika Ukumbi wa Sinodi wa Mjini Vatican , mapema Jumatatu hii , ulianza Mkutano wa kawaida wa Baraza la Makardinali. Hii ni hatua ya kwanza inayoelekea katika kumchagua Papa mpya siku za hivi karibuni, uchaguzi unaofanyika katika kikao kinachojulikana kwa jina la Conclave.
Msemaji wa Vatican Padre Federico Lombardi, akizungumza na wanahabari Jumatatu hii, ametaja idadi ya Makardinali katika kikao cha kwanza, kuwa 142 , ambao 103 ni wapiga kura. Na kwamba Makadinali wengine walikuwa wanatarajiwa kufika Roma kati ya mchana huu na kesho asubuhi.
Kikao cha Makardinali kilianza na sala ya kuomba Roho Mtakatifu awashukie “Sancte Veni Spiritus". Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Dekania ya Makardinali alitoa hotuba ya ufunguzi, na alizungumzia umuhimu wa tukio hili, na kumtaka kila Kardinali kuzingatia kiapo cha kushiriki katika mkutano huo.
Na Kardinali Tarcisio Bertone, ambaye ni msimamizi Mkuu wa kipindi hiki cha kiti kitupu cha Petro, akijulikana kwa jina la Camerlengo, alimpendekeza, Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri katika jengo la Kipapa, kutoa tafakari ya neno wakati wa kuanza kikao cha pili cha adhuhuri kwa siku hii ya Jumatatu. Na Kardinali Sodano, pia alitoa pendekezo la kupeleka ujumbe kwa Papa Mstaafu Benedikto VXI, na mapendekezo yote yalikubaliwa.
Padre Federico Lombardi na maelezo kwamba, Makardinali pia katika kipindi cha asubuhi, waliteua wasaidizi watatu wa Camerlengo, kwa mujibu wa Katiba. Na hivyo walio teuliwa watakuwa wasaidizi kwa musa wa siku tatu. Nao ni Kardinali Giovani Baptist Re, anayewakilisha Makardinali Maaskofu; Mwingine ni Kardinali Crescensio Sepe, anayewakilisha Makardinali Mapadre na Kardinali Franc Rodè, anayewakilisha Makardinali Mashemasi. Baada ya siku tatu kutateuliwa wengine watatu kushika nafasi hiyo, nao watafanya kwa muda wa siku tatu na mzunguko huo kuendelea hadi kukamilika kwa mkutano huu.
Aidha katika kipindi hiki cha asubuhi , Makardinali 13 walitoa hotuba zao fupi lakini makini. Na kwamba, kikao kimefanyika katika hali ya udugu na maelewano na uaminifu wa kusonga mbele.








All the contents on this site are copyrighted ©.