2013-03-04 09:50:59

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika maboresho ya usawa mara baada ya kukamilika kwa Malengo ya Maendeleo ya Millenia 2015


Wataalam wa masuala ya haki msingi za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa wanabainisha kwamba, kuna haja ya kuweka mbinu mkakati wakupambana na ukosefu wa usawa katika Jumuiya ya Kimataifa, mara baada ya kukamilisha Malengo ya Maendeleo ya Millenia, ifikapo mwaka 2015. Ni changamoto ya kukuza na kuendeleza haki msingi za binadamu, usawa bila ubaguzi na mchakato wa maendeleo endelevu baada ya kukamilika kwa ajenda ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia.

Wataalam wa kujitegemea 72 katika taarifa zao kwa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa wanasema, ukosefu wa usawa miongoni mwa Jamii ni kikwazo kikubwa kinachohatarisha juhudi za kukuza maendeleo na hivyo kudhohofisha jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kutafuta haki msingi za binadamu. Mapambano dhidi ya umaskini, baa la njaa, magonjwa, ujinga; utunzaji bora wa mazingira na ubaguzi dhidi ya wanawake kama Jumuiya ya Kimataifa ilivyokubaliana, matokeo yake yameanza kuonekana hasa katika kudhibiti vifo vya watoto wadogo walioko chini ya umri wa miaka mitano.

Akizungumza kwa niaba ya wataalam wenzake, Bwana Michel Forst anasema, bado kuna watu zaidi ya millioni 900, wengi wao wakiwa ni wanawake, watoto na vijana bado wanakabiliwa na baa la njaa, UKIMWI, Malaria na Magonjwa ya kuambukiza. Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kufurahia mafanikio yaliyokwisha kufikiwa wakati ambapo bado kuna mamillioni ya watu wanaoteseka. Zaidi ya watu millioni 870 wanateseka kwa kukosa hifadhi za Kijamii.

Wataalam bingwa wa masuala ya uchumi wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuibua mikakati itakayosaidia kuboresha usawa wa maendeleo ya kiuchumi, tija na uzalishaji ili kuinua utu na maisha ya watu wengi zaidi, kama njia ya kujenga na kuimarisha haki Jamii; kwa kutoa sauti kwa wale wasiokuwa na sauti!







All the contents on this site are copyrighted ©.