2013-03-04 07:35:27

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ataendelea kukumbukwa na wengi!


Waamini wengi wameshikwa na simanzi pamoja na majonzi makuu waliposikia na hatimaye kumwona Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aking’atuka kutoka madarakani. RealAudioMP3

Ni mshangao na bumbuwazi liliowashika hata wale waliokuwa wasaidizi wake wa karibu, baadhi yao walitokwa na machozi walipoliona langu kuu la Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, likifungwa na walinzi kutoka Uswiss wakifunga virago kurudi mjini Vatican kwa ajili ya kuwahudumia Makardinali wanaoendelea na mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya!

Familia ya Mungu inaendelea kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa mchango mkubwa uliotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita wakati wa uongozi wake. Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya. Ataendelea kubaki katika historia ya Kanisa kwa kuliwezesha Kanisa kupata mwelekeo mpya unaowachangamotisha kutafuta yale mambo ya msingi; yaani kumfahamu kwa kina Yesu Kristo na kutolea ushuhuda imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Amewachangamotisha Waamini na wasomi, kujikita katika hija ya kumtafuta Mungu, maadamu anapatikana, ili kwa pamoja kuweza kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima, haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mataifa. Hiki ndicho kiini cha Mkutano wa Wakuu wa Dini na Madhehebu mbali mbali uliohitimishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita mjini Assisi, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 25 ya Maadhimisho haya yalipofanywa kwa mara ya kwanza na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili. Ni utafiti unaowashirikisha hata wale wasioamini, lakini ndani mwao wana chembe chembe ya ukweli wa maisha ya kiroho.

Anaendelea kuwaalika wasomi na wanazuoni kuhakikisha kwamba, wanasafisha na kuyapanua mawazo yao, ili waweze kupata fursa nzuri zaidi ya kukutana na Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Wakristo wanahimizwa kuendeleza ile hija ya kukutana na Yesu Kristo kwa njia ya Sala, Tafakari ya kina ya Maandiko Matakatifu, Matendo ya huruma yanayoonesha ile imani tendaji, daima wakiwa makini kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili katika vipaumbele vya maisha.

Askofu Mkuu Fisichella, anakiri kwamba, kuna baadhi ya watu katika Jamii walimbeza na kumdharau Papa Benedikto wa kumi na sita, tangu wakati ule tu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, wakisema ni “Mhafidhina” “Mtu asiyependa mabadiliko” “Mtu aliyepitwa na wakati”. Lakini, kadiri wakati ulivyokuwa unazidi kuyoyoma wale waliokuwa na mawazo mgando walianza kuona na kushuhudia cheche za mageuzi zilizokuwa zinatolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Kitabu cha Yesu wa Nazareti, ambacho kimsingi ni tafakari ya kina ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ni mchango wake binafsi kwa Kanisa! Hapa alitoa mwanya kwa wasomi kuchangia mawazo yao kama sehemu ya mchakato wa kuendelea kumfahamu Yesu wa Nazareti.

Itakumbukwa kwamba, Papa Benedikto wa kumi na sita, ni kati ya wadau wakuu wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Katika kipindi hiki cha miaka minane ya utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ametoa mwaliko kwa Familia ya Mungu, kusoma, kutafakari na kumwilisha tena Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kuzama katika undani wa mawazo ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kamwe waamini wasiyachukulie Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican juu juu, bali wazame kwa kufanya tafakari ya kina, huku wakiendelea kusoma alama za nyakati.

Benedikto wa kumi na sita, alijikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, akafaulu kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa Dini, Makanisa na Madhehebu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ameonesha heshima na nidhamu kwa imani za dini nyingine kwa kuheshimu maeneo yao ya Ibada kama alivyofanya kwa kuingia Msikitini na kwenye Sinagogi bila viatu. Hiki ni kielelezo cha unyenyekevu wa hali ya juu, uliokuwa umefumbatwa katika upole na uhalisia wa maisha yake; kipaji ambacho wengi pengine walishindwa kukitambua!

Baada ya kutangaza nia na utashi wake wa kung’atuka madarakani kutokana na umri na afya yake; kumekuwepo na mafuriko ya habari za uvumi na kashfa kiasi cha kuvuruga ukweli wa mambo, kwa kusema kwamba, alikuwa eti anaukimbia Msalaba! Lakini mwenyewe amefafanua kwa macho makavu kabisa kwamba, hana lengo la kuukimbia Msalaba, kwani daima ataendelea kushikamana kwa dhati na Kristo pamoja na Kanisa lake kwa njia ya Sala na Tafakari ya kina, kwani kwa sasa anapanda Mlimani ili kukutana na Kristo na wala si kukimbia matatizo na changamoto za dunia! NI uamuzi mgumu unaoonesha upya na ambao mtu asipokuwa na jicho la imani anaweza kupigwa butwaa!

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alitambua kwamba, Yeye ni mhudumu tu katika Shamba la Bwana, lakini, Kanisa ni mali ya Kristo; waamini wanapaswa kumfuasa ili awaongoze katika hija inayokwenda kwenye uzima wa milele. Papa Benedikto wa kumi na sita, amebadilisha mwelekeo wa kulihudumia Kanisa, sasa kama Mstaafu anajikita zaidi katika Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; mambo yanayofumbata ukimya! Ataendelea kuwa miongoni mwa Familia ya Mungu anasema, Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya kwa njia ya Sala!








All the contents on this site are copyrighted ©.