2013-03-02 10:01:56

Wanamkumbuka Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI


Waamini wa Kanisa Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaendelea kusali kwa ajili ya kummshukuru na kumwombea Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika hija yake ya maisha baada ya kuliongoza Kanisa la Kristo kwa miaka minane. Waamini wameanza kusali pia kwa ajili ya kuwaombea Makardinali wanaoanza mchakato wa kumchagua Papa Mpya.

Tukio la kung'atuka kutoka madarakani kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita limevuta hisia za watu wengi ambao wameguswa kwa namna ya pekee kwa uamuzi wa kishupavu na busara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Askofu mkuu Robert Zollitsch, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshuruku Mungu na kumwombe Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ibada ambayo ilihudhuriwa pia na viongozi waandamizi kutoka Shirikisho la Wananchi wa Ujerumani. Ibada kama hii pia imeadhimsihwa kwenye Kanisa kuu la Mama Yetu wa Yamoussoukro, Pwani ya Pembe kwa kumkumbuka Baba Mtakatifu kwa mchango wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika.

Baadhi ya viongozi wa kidini wameendelea kutambua mchango wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, unojitambulisha kwa namna ya pekee kwa ukanimungu na mawazo mepesi mepesi yasiyopenda kumwajibisha mtu katika undani wake. Baba Mtakatifu ametoa mchango mkubwa katika majadiliano ya maisha ya kiroho, Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza na mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu akiheshimiwa na kuthaminiwa!

Huu ni ushuhuda kutoka kwa Rabi Arthur Schneier, Rabi mwandamizi, aliyekuwa bega kwa bega na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Marekani kunako mwaka 2008. Anasema, uamuzi wa kung'atuka kutoka madarakani umefanywa na mtu mwenye imani thabiti, ukweli na uwazi; unyenyekevu na ujasiri mkuu.

Kwa upande wake Mustafa Ceric, Mufti mkuu wa Muungano wa Waamini wa Dini ya Kiislam nchini Bosnia anasema, baada ya kutolewa ufafanuzi wa kina kwa kile kilichoonekana kuibua hasira ya waamini wa dini ya Kiislam wakati wa hotuba ya Papa Benedikto wa kumi na sita nchini Ujerumani; ukawa ni mwanzo wa mchakato wa kutaka kujenga na kuimarisha ushirikiano wa dhati kati ya Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo, wote wakiwa na mtazamo chanya.

Walitakiwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; haki na amani duniani, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mungu mmoja na tofauti zao za kiimani zisiwe ni chanzo cha kinzani na migogoro isiyokuwa na tija! Kielelezo cha mchakato huu ni ile barua ilyoandikwa na kutiwa sahihi na wasomi pamoja na wanazuoni 138 wa dini ya Kiislam.







All the contents on this site are copyrighted ©.