Pete ya mvuvi iliyotumiwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuhifadhiwa!
Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, ukarabati wa Kikanisa
cha Sistina kitakachotumika kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya bado haujaanza
na kwamba, kwa sasa inatakiwa idhini kutoka kwa mkutano wa Makardinali unaoanza kikao
chake cha kwanza, Jumatatu, tarehe 4 Machi 2013, asubuhi.
Chumba cha kitume
kilichokuwa kinatumiwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa sasa kimefungwa rasmi baada
ya kukamilisha taratibu zote kadiri ya sheria za Kanisa. Ile Pete ya Mvuvi iliyokuwa
inatumiwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita wakati wa uongozi wake haitavunjwa
na badala yake itahifadhiwa kwenye Msalaba, kiasi kwamba haitaweza kutumiwa tena,
kama walivyofanya kwa Pete ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ambayo kwa sasa imehifadhiwa
pia kwenye kioo maalum.
Padre Lombardi amefafanua kwamba, kuna Makardinali
75 wanaoishi na kutekeleza utume wao hapa mjini Roma. Makardinali 66 hadi kufikia
Jumamosi walikuwa wamekwisha wasili mjini Roma na tayari wamekwisha wasiliana na Dekano
wa Makardinali Angelo Sodano. Baadhi ya Makardinali wasiokuwa na haki ya kupiga wala
kupigiwa kura wameonesha nia ya kutoshiriki katika mkutano wa Dekania ya Makardinali
hasa kutokana na sababu za kiafya na uzee.
Kila siku jioni katika Maadhimisho
ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, waamini
watasali Kanuni ya Imani pamoja na Sala maalum zilizotayarishwa kwa ajili ya kuwaombea
Makardinali wakati huu wanaposhiriki katika mchakato wa kumchagua Papa Mpya.