Uongozi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika kipindi cha miaka minane,
umeacha chapa ya kudumu katika mioyo ya watu wengi. Ni tukio la kihistoria katika
maisha na hija ya Mama Kanisa. Imekuwa ni fursa makini kwa watu kutambua ubinadamu
na maisha ya kiroho ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Wengi wameimarishwa
katika imani kutokana na unyenyekevu unaofumbatwa katika maisha na imani.
Ikiwa
kama Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alitoa ushuhuda thabiti wa imani yake mbele ya
macho ya bahari ya watu duniani kutokana na imani na uvumilivu katika ugonjwa; Ratzinger
kwa upande wake ametoa ushuhuda wa ushujaa unaofumbata utashi wa kukubali kwake kung'atuka
kutoka madarakani kutokana na uzee, baada ya kufanya tafakari ya kina mbele ya Mwenyezi
Mungu kuhusu dhamana na wajibu wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Viongozi
hawa wawili wametoa mfano wa kuigwa si tu kwa njia ya Mafundisho yao, bali katika
uhalisia wa maisha, uliopania daima kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika
huduma na mazingira magumu ya maisha ya mwanadamu. Uamuzi wake wa kung'atuka kutoka
madarakani si kitendo cha kukimbia utume na waamini waliokuwa wamekabidhiwa kwake
kama Kiongozi mkuu. Ni mwaliko wa kuendelea kujiaminisha mbele ya Mungu na Kanisa,
kwani Mungu mwenyewe ataendelea kuliongoza Kanisa lake.
Kwa unyenyekevu na
utulivu wa ndani, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, anasema, amejitahidi
kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao ya Kanisa, ambalo ni mali ya Mungu linaloendelezwa
kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, ili kuishi, kukua na kuamsha dhamiri za watu. Kung'atuka
madarakani kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ni mwaliko na changamoto
ya sala na uwajibikaji wa wengi.
Kwanza kabisa ni dhamana na wajibu wa Makardinali
waliopewa dhamana ya kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama ilivyo pia kwa Kanisa
zima linalopaswa kuwasindikiza Makardinali kwa njia ya sala ili kumchagua Papa Mpya
atakayesimama kidete kutangaza Injili ya Kristo, kwa mafao ya Kanisa na Ulimwengu
pamoja na kuiongoza Jumuiya ya Waamini kwa uaminifu wa Injili ya Kristo. Hii ni kutokana
na ukweli kwamba, Baba Mtakatifu peke yake hawezi kutekeleza yote!
Padre Federico
Lombardi katika tahariri yake anasema, hata wao watafanya kwa kuungana na Baba Mtakatifu
mstaafu anaendelea kusali na kutafakari kwa ajili ya Kanisa. Asante sana Baba Mtakatifu
Benedikto XVI!