2013-03-01 07:35:50

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Kwaresima


Mpendwa mwana wa Mungu, tunaendelea na tafakari yetu ya Neno la Mungu, Dominika ya tatu kipindi cha kwaresima mwaka C, Neno la Mungu likiendelea kutualika kufunga kwa ajili ya kubadilika katika mwenendo wa maisha yetu ya kiroho, kuelekeza macho yetu ya kiroho kwa Mwenyezi Mungu ambaye kadiri ya Injili ya Luka ni mwenye huruma isiyo na mfano. RealAudioMP3

Mwinjili anakazia wazo la Kuongoka, maana yake kuondokana pia na mawazo ya Mungu anayeadhibu na kumpokea Mungu wa Yesu, aliye upendo upeo, asiyemwacha mwanadamu katika udhaifu wake bali anayemwongoza afikie uzima wa milele. Anatualika nasi pia kushuhudia upendo wa Mungu yuleyule anayetupenda kwa ajili ya wengine. Tunaalikwa basi kuongoka, maana yake kuzaa matunda ya mapendo ambayo mpaka sasa hatujaweza kuyazaa.

Mungu ametuachia muda wa kutosha kama mwenye bustani ya dhabibu alivyoacha kuukata mdhabibu na hali akiendelea kuumwagilia maji na kuulisha mbolea ili baadaye uzae matunda, la usipozaa basi kwa hakika haki inasonga mbele!. Hapa tayari ndugu yangu mpendwa unaonja fadhila ya uvumilivu wa Mungu na ambayo nawe wapaswa kuitafuta toka kwa yule anayeitoa naye ni Mungu mwenyewe.

Katika Injili tunamwona Yesu Kristo anayesahihisha mawazo potofu juu ya uhusiano wa dhambi na kifo ambao unapelekea kumwona Mungu kama ni yule anayeadhibu badala yakuwa yule anayewapenda viumbe vyake. Mara moja Bwana anasema kifo cha Wagalilaya ambao tumewasikia katika Injili hakina uhusiano na dhambi zao, kumbe, Mungu ni upendo. Akisha kusema hilo anakuja na hoja nzito juu ya nini cha kushika kwako wewe unayenisikiliza. Anasema tena akirudia mara kadhaa “lakini msipotubu , ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo”.

Kumbe mpendwa mwana wa Mungu, wito kwako leo ni toba na wala si kuangalia maangamizi, njaa, vita, kama ni matokeo ya dhambi ya yule anayeteseka. Bwana hayuko katika kuwaadhibu watu bali kuwapenda na kushiriki mateso yao na hatimaye kuwaokoa. Mwandishi mwanabiblia Daniel Marguerat aliwahi kusema kwamba Yesu Kristu hakuwa na hakuwahi kuwa na mahubiri ya kijasusi yaani yanayotishia maisha ya watu, au mahubiri ya jino kwa jino bali yaliyojaa huruma na mapendo.

Tunaweza kusema Bwana anasisitiza WONGOFU wa ndani, na kadiri ya Injili ya Dominika hii ni kuondokana na picha ya Mungu wa kipagani, Mungu aliye hakimu na kwa njia ya hiyo basi tutakutana na Mungu aliye upendo ambaye Bwana anatuwekea mbele yetu anapofanya majadiliano na watu waliomfikia katika Injili.

Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto anawaonya pia katika nia ya kuwasaidia wakumbuke jambo la msingi ni kubadilika na kumwongokea Mungu. Ndiyo kusema, ubatizo pekee hautoshi bali unaambatana na matendo ya upendo na udumifu katika ubatizo huo. Anakuja na mfano wa Waisraeli jinsi ambavyo waliokolewa na Mungu toka Misri mpaka nchi ya ahadi lakini wengine kwa sababu ya kiburi chao wenyewe walipotelea njiani.

Mungu aliweka kila aina ya nyenzo ili wafike kwenye nchi yao lakini wengine waliaanza hata kukumbuka nyama za huko Misri na kusahau mateso yao. Mpendwa msikilizaji jambo la upendo wa Mungu liko wazi na kila mmoja wetu ni mrithi lakini pasipo kuwajibika na hasa kwa kuishi maisha ya kiinjili hakutakuwa na nafasi, kama vijana wetu wanavyosema patakuwa hapatoshi!

Mpendwa msikilizaji, ninakukumbusha kuwa ukristu wa Jumapili hautoshi bali ukristu kuanzia maisha ya pamoja katika familia, ujirani mwema, Jumuiya Ndogondogo, Kigango, Parokia, Jimbo hadi Kanisa la Kiulimwengu chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kumbe Mt. Paulo anaposema mambo yaliyowatokea Waisraeli huko safarini yawe ni maonyo kwetu, anataka kutuambia kuweka bidii katika maisha mazima ya kumwongokea Mungu.

Katika somo la kwanza tunamwona Musa ambaye anaitwa na Mungu kuongoza taifa la Israeli toka utumwani Misri. Kwanza Mwenyezi Mungu anajifunua na kuonesha ukuu wake kwa Musa na kwa namna hiyo kwetu. Anasema “Mimi niko ambaye niko” Baada ya kujionesha Musa anasema mimi hapa! Na hivi yu tayari kutumwa. Kwanini Mungu anamtuma Musa? Neno lake linatuambia, “hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimesikia kilio chao” Mara moja Mungu anaona si vema kuwaacha watu wake aliowaumba wabaki katika mateso bali washiriki mapendo aliyowatayarishia tangu mwanzo.

Ndiyo kusema kwetu sisi leo Mungu yuko pamoja nasi katika shida zetu kama Bwana asemavyo katika Injili ya Matayo 28:28 na kuendelea, nipo pamoja nanyi mpaka ukamilifu wa dahari. Lililo la msingi hata hivi leo ni mwondoko mtakatifu kwenda kwake daima kwa njia ya sakramenti za Kanisa na hasa Kitubio. Mkristu ni yule anayetubu dhambi zake na kuishi upendo kwa ajili ya wengine. Mkristu ni yule ambaye anatambua kuwa Bwana amejaa huruma na neema kama tunavyosikia katika wimbo wa katikati dominika hii.

Tuseme nini mpendwa zaidi ya kuendelea kufurahia msamaha wa dhambi na upendo upeo tunakirimiwao na Bwana kila siku ya maisha yetu tukialikwa kuongoka. Na kwa namna hiyo nikutakie Kwaresima njema na tafakari njema ya Neno la Mungu kila siku ya maisha yako.Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.